WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kwa wanachama wake wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini, ameona hana budi kutangaza rasmi azma yake.
Dk. Magufuli, mmoja wa mawaziri ambao kwa muda mrefu wamehusishwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo, alisema anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga na kupigiwa kura.
Alitangaza azma yake nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu bungeni, jana asubuhi.
Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo, mara moja alisema: “Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza.
“Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea urais’. Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema siku ya kuchukua fomu ataitangaza baadaye pindi akishakamilisha taratibu za namna ya kuanika hadharani mambo anayokusudia kuyatekeleza endapo wana CCM watampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho.
Kuingia kwake kwenye harakati za kuwania nafasi ya urais kunazidi kuufanya mchuano wa uchaguzi wa nafasi hiyo ndani ya CCM kwa mwaka huu kuwa mkali zaidi.
Dk. Magufuli, amekuwa mbunge tangu mwaka 1995. Baada ya kushinda ubunge mwaka huo, alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi; Wizara iliyokuwa ikiongozwa na Anna Abdallah.
Anajulikana kama kipenzi cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa, ambaye mara kadhaa hakusita kumsifu hadharani, akimtaja kama mmoja wa ‘askari wa miavuli’ katika baraza lake la mawaziri.
Aidha, uhusiano wake na Mkapa umejidhihirisha hadi kwenye masuala ya kifamilia, ambako mara kadhaa rais huyo mstaafu ameweza kuhudhuria hafla na misiba mbalimbali nyumbani kwa Dk. Magufuli.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk. Magufuli alipewa fursa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM kusoma mafanikio ya chama hicho kwenye utekelezaji wa ilani yake upande wa barabara.
Uwezo wake wa kukariri takwimu mbalimbali, ulikuwa kivutio kwenye mkutano huo na sehemu nyingine kama bungeni ambako hutakiwa kueleza mafanikio ya wizara yake.
Hivi karibuni, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Ali Hassan Mwinyi, alimsifu kwa kumtaja kama ‘simba wa kazi’ kutokana na uchapaji kazi wake katika wizara mbalimbali ambazo ameziongoza.
Kwa upande wa wananchi, wengi wanamuona Dk. Magufuli kama mmoja wa mawaziri wachapakazi waliowahi kutokea katika historia ya taifa hili.
Hata hivyo, waziri huyo amekuwa akikosolewa kwa uamuzi wake wa uuzaji nyumba za Serikali kwa watumishi na hata wasio watumishi wa umma.
Pamoja na dosari hiyo, watetezi wake wanaamini kilichofanywa wakati huo wa utawala wa awamu ya tatu kilikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Baraza la Mawaziri, na si uamuzi wa Dk. Magufuli mwenyewe.
WASIFU WAKE
Dk. John Pombe Joseph Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato – wakati huo ikiwa Mkoa wa Kagera (sasa Mkoa wa Geita).
Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 1991 – 1994, alisoma Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza.
Mwaka 1985 – 1988, alisoma Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1981 – 1982, alisoma diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1979 – 1981, alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa, Iringa.
Mwaka 1977 – 1978, alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza.
Mwaka 1975 – 1977, alisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera.
Mwaka 1967 – 1974, alisoma Shule ya Msingi, Chato.
Mafunzo
Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma.
Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha.
Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma.
Uzoefu wa kazi
Mwaka 2010 – hadi sasa: Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato.
Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki; Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato).
Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato)
Mwaka 2000 – 2005: Waziri wa Ujenzi, na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1989 – 1995: Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.), Mwanza.
Mwaka 1982 – 1983: Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati).
Dk. Magufuli amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa. Ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Ameoa na ana watoto kadhaa.