27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim seif ajitosa urais mara tano

ESTHER MBUSSI NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR
MAKAMU wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amejitosa tena kwa mara ya tano kuchukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar.
Kutokana na hatua hiyo amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kijiandae kisaikolojia kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), itakayoongozwa naye huku akisema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ndiyo utaamua hatima yake kisiasa.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu wa CUF, aliyasema hayo jana mjini Unguja, baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi za CUF Wilaya ya Magharibi.
Alisema uamuzi huo wa kuiongoza SUK utatokana na ridhaa ya wananchi wenye kiu ya maendeleo ya muda mrefu iliyoshindwa kutekelezwa na CCM, licha ya chama hicho kuanza njama chafu za kuwakosesha wanachama wa CUF vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, huku wao wakiwaandikisha watu walio chini ya umri unaotambulika kisheria.
“Wananchi wakiamua Maalim Seif aingie Ikulu, hakuna chama, taasisi au mtu wa kutengua maamuzi hayo, najua nimebeba matumaini ya vijana, wanawake, wanaume na vichanga wote wa Zanzibar, wananchi bado wana kiu ya kupata uongozi ambao utakidhi matakwa ya wananchi wa rika zote.
“Urais ni mzigo mzito, lakini kwa sababu nina uhakika sitaubeba peke yangu nitaubeba pamoja na ninyi, basi utakuwa rahisi na tutakwenda hatua kwa hatua ili kuona Zanzibar inakuwa na maendeleo ya kisasa,” alisema.
Hata hivyo, Maalim Seif aliwataka wananchi kuamua kwa kura zao hususani vijana ambapo pia aliwasisitiza kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho vya ukaazi.

Kugombea mara ya tano
Pamoja na mambo mengine, Maalim Seif alisema baada ya uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba mwaka huu, ndiyo ataamua kama ataendelea kugombea urais nafasi ambayo amekuwa akiiwania tangu mwaka 1995.
“Hili suala la mimi kugombea kila siku au kama nikishinda au kushindwa nitafanya nini, uchaguzi wa mwaka huu ndiyo utaamua hatima yangu kisiasa.
“Na pia muelewe wanachama wa CUF si waoga kutoomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea urais isipokuwa wamekuwa wanaona ninafaa, si kwamba ni waoga eti wananiogopa mimi, hapana pengine wanaona Maalim anatosha na anafaa kwa nafasi hiyo.
“CUF hakuna suala la woga, haki sawa kwa wote, suala la kugombea nafasi zote liko kwenye katiba na mwanachama yeyote anayo haki ya kugombea nafasi yoyote, sasa ukiniuliza kwanini wengine hawagombei mimi sijui,” alisema Maalim Seif
Alisema wananchi wote watakaojitokeza katika kinyang’anyiro hicho majina yao yatapelekwa katika Baraza Kuu la chama hicho ambalo litamteua mtu mmoja atakayeonekana anafaa kupeperusha bendera ya urais.

Vipaumbele vipya
Katibu Mkuu huyo wa CUF, alisema safari hii akiingia madarakani atahakikisha kunakuwa na amani, haki, umoja na mshikamano.
Alisema wananchi wana kiu ya kuona Zanzibar inakuwa na amani ya kweli, umoja wa kweli na usalama wa kweli kwa kushirikiana na viongozi wao.
“Cha muhimu katika nchi ni kuwa na umoja na haki, naamini sasa hivi hakuna haki, kuna ubaguzi ndiyo maana wanachama wetu wa CUF hawapewi vitambulisho vya ukaazi, lakini wengine wanapewa, mwenye haki hapewi,” alisema.

Matumizi ya fedha
Kuhusu matumizi ya fedha wakati wa kampeni na uchaguzi kwa ujumla, alisema chama chake kimekuwa kikiingia kwenye kampeni bila kuwa na fedha kwani hawana wafadhili.
Alisema kampeni zake zitaendeshwa na jeshi la wanachama wa chama hicho ambao wameamua kuungana kwa pamoja kushirikiana naye kwa kila jambo na wanatoa michango yao itakayosaidia kufanikisha kampeni hizo.
“Tangu mwaka 1995 tumekuwa tukiingia kwenye uchaguzi hatuna shangazi, mjomba wala mfadhili, tunaamini kinachohitajika ni jeshi la wananchi ambao ndio wapigakura.
“Sisi hatuna fedha, hata hizi shilingi 500,000 za kuchukulia fomu nimechangiwa na wanachama, kama wenzetu wana fedha basi sisi hatuna,” alisema.

Kugombea na Dk. Shein
Hata hivyo, akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kugombea na Rais Dk. Ali Mohamed Shein, alisema haoni tatizo na kwamba angekuwa yeye ndiyo rais angesisitiza uchaguzi huru na wa haki.
“Ningekuwa mimi ndiyo rais nisingeiba kura, kutumia mabavu wala nguvu katika uchaguzi mkuu huu, wananchi waachwe waamue,” alisema.

Afya yake
Kuhusu afya yake, Maalim Seif alisema yuko imara kimwili, kifikra na kiakili ndiyo maana akapata msukumo wa kuendelea kugombea kwa lengo la kutekeleza malengo aliyowaahidi wananchi kwa muda mrefu.
“Mimi naamini ni mzima kimwili na kiakili na kwa kuthibitisha hilo ninawaalika ninapofanya mazoezi mje kuniona,” alisema.

MAALIM SEIF NI NANI?

Maalim Seif Sharif Hamad ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyezaliwa Oktoba 22, mwaka 1943, katika Kijiji cha Nyali, Mtambwe kisiwani Pemba.
Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Uondwe, 1950 na baadaye alijiunga na elimu ya sekondari katika skuli ya watoto wa kiume, Wete Pemba mwaka 1952.
Baadaye aliendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya King George na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1963 na kati ya mwaka 1972 na 1975 alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa (Political Science).

Kazi
Kati ya mwaka 1972 na 1975 alifundisha katika shule mbalimbali za Unguja na Pemba, zikiwamo Fidel Castro na Lumumba

Siasa
Maalim Seif alianza kuingia katika masuala ya siasa, ambapo 1977 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Mwaka 1977 hadi 1987, alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Mwaka 1982 hadi 1987 alikuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya CCM na mwaka 1984 aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi mwaka 1988.
Baada hapo, misukosuko mikubwa ya kisiasa ilianza kumkumba ambapo Januari 1988 alipoteza nafasi ya Uwaziri Kiongozi na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi baada ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Idrisa Abdulwakil kutangaza kulivunja Baraza la Mawaziri.
Mei 1988, Maalim Seif alitoka katika chama cha CCM.
Agosti 16, mwaka 2010 alichukua fomu kuwania urais wa Zanzibar kwa awamu ya nne kupitia chama cha CUF na jana Mei 28, amechukua fomu ya ndani ya chama hicho kuwania tena urais kwa mara ya tano.

Abebeshwa msalaba
Alipojitokeza mwaka 2010 kuwaomba Wazanzibari ridhaa yao ili aweze kuiongoza Zanzibar Mpya waliyoazimia kuijenga, aliahidi kutekeleza matakwa ya Katiba ya Zanzibar kama ilivyorekebishwa kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Pamoja na kutoa ahadi hiyo mwanasiasa huyo ambaye kila kukicha amekuwa akionekana kuwa ni mwiba kwa CCM, hivi sasa anabebeshwa msalaba hasa baada ya wabunge na wawakilishi kutoka kwenye chama chake cha CUF kuonekana ni wahafidhina na hawana nia njema kwa masilahi ya taifa juu ya kupatikana kwa Katiba Mpya.
Ahadi yake ilikuwa ni kuuimarisha Muungano kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri na kujenga uchumi imara kwa kuzingatia mfumo wa soko huria unaotoa fursa ya ushiriki kwa wananchi wote na ambao unaratibiwa vyema na Serikali hasa kupitia sekta za kilimo, uvuvi, utalii, biashara na viwanda ambazo zitapewa kipaumbele katika ujenzi wa uchumi wa kisasa wa Zanzibar Mpya.
Kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi serikalini na ubora wa huduma zinazotolewa na utumishi wa umma kwa kusimamia ipasavyo kanuni za kazi, kuwapatia mafunzo ya kazi na kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake ya kituo kikuu cha biashara na huduma katika eneo lote la Afrika Mashariki.
Sasa anatupa kete kwa mara ya tano kutaka kuiongoza Serikali ya awamu ya nane ya Zanzibar. Je, atafanikiwa kuzishinda harakati zinazofanywa za kutaka aonekane ni mmoja wa wanasiasa waliopotea hasa baada ya kuingia katika Serikali ya pamoja ya SUK?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles