Na ELIZABETH HOMBO-ARUSHA
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameishauri Serikali kujitathmini kupitia mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani zinazoendelea nchini.
Mbowe ambaye pia n mbunge wa Hai, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na MTANZANIA kuhusu hamasa ya wananchi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani.
Alisema mikakati yote inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano, ikiwamo kujenga viwanda, wananchi wa kawaida hawaoni faida.
Kutokana na hilo, alisema matokeo yake Serikali na chama chake wanakwenda kushoto, huku wananchi wakienda kulia.
“Reform (mabadiliko) zote zinazohubiriwa na rais pamoja na mikakati yote, ikiwamo kujenga viwanda, hakuna mwananchi yeyote anayeona lina faida kwake.
“Katika mazingira hayo, rais na Serikali yake pamoja na chama, wanaonekana wanakwenda kushoto, huku wananchi wakienda kulia, hawaelewi.
“Watu wanaugulia mioyoni, hawasemi kwa sababu wakisema hawana uhakika wa maisha yao, hivyo wanakaa kimya wakiumia.
“Hilo unaweza kuliona katika mikutano hii, si mashabiki wa Chadema tu wanaohamasika kuhudhuria, bali wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama… ni vyema sasa Serikali ikajitathmini,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, taifa lilikumbwa na ganzi, huku wananchi wakibaki na maswali mengi juu ya hatima ya taifa.
Alisema baada ya hapo, majukwaa mawili muhimu ya kuwapa taarifa wananchi, Bunge na mikutano ya hadhara, yalizuiwa.
“Hivyo sintofahamu ya wananchi ilikuwepo na haijapata majibu hadi kipindi hiki, lakini kwa kiwango kikubwa wananchi wamekuwa wakisikiliza upande mmoja tu.
“Hata bungeni kikizungumzwa kitu kinachujwa, wakati huo huo walichoambulia wapinzani na wafuasi wao ni kamatakamata,” alisema Mbowe.
Alisema hamu kubwa ya wananchi katika mikutano ya kampeni ya uchaguzi mdogo, imechangiwa na kukaa miaka miwili bila mikutano ya hadhara.
Mbowe alisema pamoja na matukio yote, kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za maisha.