32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI KUFUTA MATUMIZI YA DOLA NCHINI NI SAHIHI

Na Shermarx Ngahemera

KWA Watanzania wa umri wa makamo  watakumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa anaziita fedha zetu za shilingi kama fedha za madafu  sio kwa kuzidharau  ila  kwa kuonesha kuwa zinapatikana kwa wingi nchini lakini haziwezi kununua  bidhaa  na huduma nje ya mipaka yetu.

Sarafu ya nchi ni kitu  adhimu na muhimu sana kama kitambulisho cha utaifa, uhuru na dola husika kwani ni nchi tu ndio zimeruhusiwa kuwa  na  sarafu na fedha zake kwa kutambua umuhimu wa kukubalika kwa matumizi ya watu wa nchi hiyo na hivyo kuwafanya watu wa mataifa mengine kukubali kutumia fedha hiyo kwani wanajua kwa vyovyote vile itakubalika katika nchi hiyo, na hivyo kubeba thamani na dhamana katika maduka ya fedha na uchumi.

Mwalimu Nyerere alikuwa anazizima akimkuta Mtanzania na fedha ya nje kwani kulikuwa na sheria kali juu ya umiliki na matumizi ya fedh za nje kwani zilikuwa zinaonesha mapungufu fulani kwa mhusika. Nyerere alikuwa anaita  hali hiyo kasumba ya Magharibi na hivyo mtu huyo alihesabika kuwa sio Mzalendo. Uzalendo ni pamoja na mtu kuheshimu  sarafu ya nchi yako ambayo viongozi wameweka saini zao kusema kuwa ni fedha halali kwa matumizi yaliyoainishwa nchini.

Kwa miaka ya karibuni kuanzia utawala awamu ya Tatu na haswa baada ya vurugu za  ubinafsishaji  kukazuka matumizi holela ya dola za Marekani kiasi kwamba yalikuwa yanakera na kuleta ubaguzi ndani yake.

Tokea hapo imekuwa ni jambo la kawaida maeneo mengi sana ya kiuchumi na serikali yenyewe ikishabikia  matumizi hayo ambayo hayakuwa  ya kisheria  kwani yalikatazwa  lakini hakuna  aliyesikia na hivyo kuwa na mfumo sambamba  wa sarafu yaani shilingi  kwa mafukara na Dola kwa matajiri hali ambayo ilisaidia kwa kiasi kikubwa kudidimiza uchumi wan chi kwa kuendeleza matamanio ya vya nje.

Watengenezaji , walinzi na watawala wa fedha zetu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hawakujali  na walipoulizwa walisema bila kumung’unya kuwa matumizi hayo (dollarization of the economy)  yalikwa sahihi  na yanafaa na kuhitajika ili watu  waweze kuzoea Dola za Marekani ambayo ilipewa jina kama fedha ya Dunia.

Kwa vile somo la uchumi sio sayansi timilifu watu waligawanyika misimamo na wote kuwa sahihi kuhusu matumizi ya dola na athari zake kiuchumi lakini kiwango cha ubadilishaji wa dola na shilingi ilizidi kuinanga shilingi yetu mpaka  ikakosa thamani na hali yetu ya uchumi ikawa  kitendawili.  Kimsingi huwezi kuwa na uchumi unaokua kwa asilimia 7 na huko kila siku shilingi yako inazidi kupungua thamani;  hii ilitokana  na mahitaji yasiyo ya msingi ya Dola kutoka na uholela wa sera zetu.

Kuficha aibu ya kipigo cha shilingi yetu ikawekwa kwenye kapu la fedha (basket of six currencies) kali  zikiwamo Dola ya Marekani, Pauni ya Uingereza, Yen ya Japan, Guilder ya Uholanzi, Euro ya Ulaya na kufanya ielee humo (floatation) sio kama meli bali kama mtumbwi uliosulubiwa na mawimbi ya bahari ya sarafu.

Sasa ni muafaka kwa wachumi wetu kutoa elimu kwa umma juu ya athari zote hasi na chanya juu ya kauli hiyo ya rais  na kutoa matokeo mbalimbali kwa wananchi kuelewa umuhimu na thamani ya kutumia shilingi ya Tanzania.

Japokuwa  katika mazingira ya kawaida na kuna matokeo ya utafiti yanayoelezea kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi, hakusababishwi na bidhaa kutozwa kwa dola, lakini umefika wakati wa kuona kitendo cha kushamiri kwa ununuzi wa bidhaa kwa dola ni aibu kwa watu  huru wan chi husika kwa kukosa utambulisho  wa uchumi wenu na hivyo kutoheshimiwa kwenye mambo mengine hasa ikitiwa maanani kuwa sarafu ni kielelzo na kigezo cha mapato na matumizi katika uchumi husika na hivyo sio jambo la mchezo. Maeneo mengine walipiga marufuku matumizi ya shilingi ya Tanzania! Ukicheza na mbwa utaingia naye msikitini.

Hii inatokana na misingi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi, pamoja na hali halisi ya uchumi wa nchi zinazofanya biashara na Tanzania, japokuwa nakisi ya urari wa biashara , mfumuko wa bei na tofauti ya misimu, inazosababisha kushuka na kupanda kwa thamani ya shilingi ni vitu vya kuzingatia kama nchi.

Hivi basi kauli ya Rais Dk. John Magufuli kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ijipange katika kuhakikisha matumizi ya dola yanaondoka kwenye ununuaji wa bidhaa mbalimbali ni jambo zuri, lakini pia ni wakati wa wasomi wetu, hasa wachumi, kwenda mbali zaidi katika utekelezaji wa jambo hilo.

Ili kusaidia kuimarisha thamani ya shilingi au sarafu, Benki Kuu ijitahidi iendelee kudhibiti mfumuko wa bei, ili usitofautiane na wabia  wetu wa biashara pamoja na kutoa maelekezo sahihi, kwa kuwa haiwezekani leo hii hata bia  katika maduka makubwa inauzwa kwa dola. Huu ni uhayawani!

Japokuwa BoT imefanya kazi kubwa ya kudhibiti biashara ya maoteo katika soko la fedha za kigeni inafanywa na benki kwa ajili ya shughuli za kiuchumi tu na siyo biashara ya maoteo (predictions).

Benki Kuu  inapaswa kuja na sheria bora itakayoweza kuzuia hili, ili kuipa heshima shilingi, ambayo kwa sasa kutumia dola imekuwa ni jambo la kawaida hata katika upangishaji wa maeneo mbalimbali.  Inasikitisha kuona kuwa hata serikali yenyewewe ikidai kulipwa Dola kutoka watu wake kwenye kulipia kodi ya pango la ardhi, malipo ya pasi ya kusafiria na tozo nyingine zote kwenye mfumo wa serikali. Ni ajabu kubwa hii kwa  mpika uji  yeye mwenyewe asiunywe au kuuonja.

Kama serikali iliinyanyapaasarafu yake nani ategememewe kuikubali na kuiheshimu na kwa mwendelezo  ni kuwa uhuru wa dola yetu ulitiliwa shaka (sovereignity of the realm)  na wenzetu na hivyo kukosa kuaminiwa nao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles