Na Shermarx Ngahemera
MAJI yanayotumika Dar es Salaam yanatoka Mkoa wa Pwani na katika mazingira tegemezi maji hayo yamehodhiwa na Dar es Salaam, kutokana na uchumi wake kuwa mkubwa na hivyo kuinyonya Pwani, mkoa ulio jirani na sasa unaochipukia kwa kasi kiuchumi.
Mkoa wa Pwani kwa miaka mingi umekuwa tegemezi kwa miundombinu yake kutokea Dar es Salaam na kuacha kushughulikia matatizo yake na hivyo kusinyaa kiuchumi hadi Awamu hii ya Tano ya Utawala .
Wajuzi wanasema hakuna marefu yasiyo na ncha na kwa hali ilivyo inabidi Pwani ijitoe kwenye kumilikiwa na Dar es Salaam kama inataka maendeleo ya haraka na ya kuaminika ya uchumi wake.
Kunaonekana kuna mgongano wa masilahi wa wazi umeanza kujitokeza katika rasilimali za msingi ikiwamo maji, ambapo Pwani inaonekana kutoridhika na mambo yanavyokwenda kwani kipaumbele hutolewa kwa Dar es Salaam badala ya Pwani mwenye maji yake kwani yanazalishwa kwenye mkoa wake.
Kuzingatia ukweli wa hali hiyo inayokosesha afya ya kiuchumi, Serikali imeitaka bila kumung’unya maneno Shirika Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kushiriki katika mfumo wa uchumi wa viwanda katika Mkoa wa Pwani.
Pia, wametakiwa kuhakikisha mkoa huo unapata maji safi na salama ili wawekezaji waweze kujenga viwanda haraka na kwa ufanisi zaidi.
Kwa maelezo ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kuna viwanda zaidi ya 300 mkoani Pwani ambavyo viko katika hatua mbalimbali za ujenzi mkoani Pwani na vitaanza kufanya kazi karibuni.
Kinachogomba ni kuwa Dawasco kama jina lake linavyoonesha limejikita zaidi kiutendaji kwa Dar es Salaam kama jiji na mkoa na hivyo maendeleo yanayofanyika mkoani Pwani si kipaumbele chake isipokuwa Bagamoyo ambayo inayo uhusiano wa kihistoria na kitamaduni na hivyo kuhusishwa katika picha kubwa ya mipango ya maji.
Wilaya nyingine mkoani Pwani zikiwamo za Rufiji, Kibiti, Kisarawe na Mkuranga hakuna maji ya Dawasco na hivyo kudai uundwaji wa kampuni mpya ya maji kwa mkoa wa Pwani ili kufikisha huduma hiyo kwa viwanda vinavyokuja kwa nguvu kubwa na kwa wakazi wa mkoa huo. Wakazi hao wanataka vilevile chanzo cha maji kibadilike na kuwa Mto Rufiji badala ya Mto Ruvu.
Ukweli unaonesha Dawasco haina uwezo wa kuhudumia Mkoa wa Pwani kwani Dar es Salaam yenyewe inawashinda kwa viwango vya hivi sasa.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandidi Isaack Kamwelwe, akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi ya tano ya wakurugenzi wa Dawasco Kibaha mkoani Pwani, alisema maji yamekuwa chanzo kikubwa kwa wawekezaji kushindwa kuwekeza kwenye viwanda kikamilifu mkoani humo.
Mhandisi Kamwelwe alilalama kuona hali mbaya ya maji Mkoa wa Pwani na kusema Kisarawe kuna mradi mkubwa wa viwanda, lakini unashindwa kuendelea kwa sababu ya kukosa huduma hiyo ya maji, lakini hakutoa suluhisho lake kwani yeye ni mhusika mkuu wa tatizo.
Alisema Juni 21, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli akiwa Kibaha, Pwani, alishatoa agizo mkoani humo kupelekwe maji safi ili shughuli za ujenzi wa viwanda uendelee.
Kamwelwe aliitaka Kampuni ya Dawasco ifikapo mwaka 2020, Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam iwe imefikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji safi na salama. Wakazi wanasema muda huo ni mbali sana na kudai leo.
Waziri Kamwele alikumbushia na kushangaa kuwa rais alishatoa agizo kupelekwa kwa miundombinu ya maji Mkoa wa Pwani, inashangaza mpaka hivi sasa kuna sehemu nyingine bado miundombinu haijafika, hali hiyo inasababisha kukosa wawekezaji.
Kwa mtazamo wa mambo, wachunguzi wanasema si rahisi Dawasco kufikiria kwa undani suala la kupeleka maji Mkoa wa Pwani, kwani wana kasumba kuwa wao kama wanavyosomeka ni kwa ajili ya Dar es Salaam na si Kibaha na hivyo kupeleka maji Kibaha ni hisani na si kipaumbele kama inavyotakikana.
Ukweli wa mambo ni kuwa mpanda ngazi na mshuka ngazi hawawezi kushikana mikono kwani ni lazima waachane ikiwa wanataka kupiga hatua. Kwani mkoa wa Pwani unapanda ngazi na Da re sa Salaam inashuka na hata kunyag’anywa Makao Makuu ya Serikali kwani yanahamia Dodoma.
“Mkoa wa Pwani ndio unaongoza kwa miradi mipya ya viwanda ambapo hivi sasa kuna viwanda 82, hivyo ni muhimu miundombinu ya maji iboreshwe ili viwanda vifanye kazi kwa uharaka ili kukuza uchumi kwa Taifa,” alisema Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Anathibitisha Mkuu wa Mkoa huyo kuwa bado kuna changamoto ya maji katika Mkoa wa Pwani, ingawa kwa mahitaji ya sasa upatikanaji maji umefikia asilimia 62.5 ya mahitaji na hivyo Dawasco wanahitajika kuongeza nguvu zaidi ili kufanikisha uchumi wa viwanda nchini.
Mahitaji ya maji yanajitokeza katika sura mbalimbali kama kipoza, malighafi na matumizi ya usafi viwandani. Wajuzi wanasema hakuna kiwanda bila maji na hivyo Dawasco wawe wakweli na waache kung’anga’ania wasichokiweza.
Kaluwa Steel Mills Mlandizi nao walilazimika kuvuta umeme kilomita 4 toka ‘substation’ na kiwanda kama Twyfords Tiles wametafuta suluhisho lake kwa kuvuta wenyewe maji toka Mto Ruvu wakati wakisubiri upatikanaji mwafaka wa maji toka Dawasco, wakati kiwanda cha Goodwill Tanzania Ceramics kilichopo Mkuranga kina mahitaji makubwa ya maji kwani kinaanza uzalishaji mapema mwakani.
Lawama hizo zinamfanya Mkurugenzi wa Dawasco, Cyprian Luhemeja, asipate usingizi na kusema kuwa upatikanaji wa maji umeongezeka kwa asilimia 75 wakati upotevu wa maji umepungua kwa asilimia 28. Awali upotevu wa maji kutokana na wizi na mtandao uliochakaa ulifikia kiwango cha kutisha cha asilimia 40. Anasema Bagamoyo iko kwenye mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na kampuni ya Kihindi.
Alisema malengo waliojiwekea Dawasco ni kuwa ifikapo 2020, asilimia 95 ya upatikanaji wa maji itakuwa imeboreshwa na ifikapo mwaka 2025 watu milioni 10 wanatakiwa kupata maji safi na salama.