Mwandishi wetu, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuweka alama ya X kwenye jengo moja la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo linahitajika kubomolewa, mamlaka hiyo imeliambia gazeti hili kuwa majengo yote yako kwenye hifadhi ya barabara.
Yako majengo mawili kwenye eneo hilo la makao makuu ya Tanesco, Ubungo, Dar es Salaam
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama, aliliambia MTANZANIA kwa njia simu jana kwamba mamlaka hiyo inaandaa notisi ambayo itapelekwa Tanesco.
Alisema kwa mujibu wa taratibu, suala la kwanza huwa ni kuandika notisi ya kubomolewa ili mhusika ajiandae kuondoka eneo husika.
“Tunaandika barua ya notisi leo hii (jana) kwa Tanesco, ambayo inatoa siku 30 za kujiandaa na kukusanya vitu kwenye jengo na kuondoka… baada hapo sisi tutaendelea na taratibu za kubomoa,” alisema Ndyamukama.
Alipoulizwa kama ni jengo moja litakalobomolewa, alisema majengo yote mawili yako katika eneo la hifadhi ya barabara.
Kwa upande wa gharama za kubomoa, meneja huyo alisema Tanroads itatathmini gharama ya kubomoa na itajulikana baadaye.
Juzi, Rais Magufuli aliitaka Tanroads kuvunja sehemu ya majengo ya Tanesco na ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji yaliyopo kwenye hifadhi ya barabara kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja la ghorofa tatu la Ubungo (Ubungo Interchange), Dar es Salaam.
Baadaye taarifa iliyotolewa na Ikulu ilimnukuua Rais Magufuli akisema, “sheria ya hifadhi ya barabara katika eneo hilo ni mita 90 kila upande kutoka katikati ya barabara.
“Hivyo ni lazima sheria hiyo iheshimiwe kuharakisha ujenzi wa daraja la ghorofa tatu katika eneo hilo la Ubungo unafanyika bila vikwazo kwa sababu sheria ni msumeno haina budi kuzingatiwa hata na serikali yenyewe”.
Rais Magufuli pia aliiagiza Tanroads kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara kutoka eneo linapoishia daraja la ghorofa tatu Ubungo kwenda Chalinze mkoani Pwani, ili itanuliwe kurahisisha usafiri Dar es Salaam.
Rais aliwataka makandarasi wanaojenga daraja la Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi wa madaraja hayo kwa kuyajenga usiku na mchana ili yamalizike kwa wakati au kabla ya muda huo kurahisisha maendeleo ya biashara katika Jiji la Dar es Salaam.
“Dar es Salaam ni jiji la biashara, hivyo hakuna budi miundombinu yake ya usafiri iweze kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya jiji na nje ya Dar es Salaam,” alisema.
Machi 20 mwaka huu, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu Ubungo utakaochukua miezi 30 hadi Septemba 2019.
Mradi huo utagharimu takriban Sh bilioni 188.71 ukiwa na lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma.
Fedha za ujenzi wa barabara zenye ghorofa tatu, umefadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo imetoa zaidi ya Sh bilioni 186.7 kwa ajili ya gharama za usanifu, usimamizi na ujenzi wa mradi wakati serikali ikichangia zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili huduma nyingine ikiwamo kulipa fidia nyumba zitakazoathiriwa na mradi huo.
Alipozindua ujenzi huo, Dk. Magufuli aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Tanroads kumsimamia mkandarasi, Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) kujenga barabara za viwango na kukamilisha ujenzi haraka.