29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

NDEGE ILIYOUA 11 ARUSHA YADAIWA KUGONGA MLIMA

SUSSAN UHINGA NA OSCAR ASSENGA, ARUSHA

MIILI ya abiria 11 waliokua kwenye ndege ya Shirika la Coastal Aviation iliyoanguka jijini Arusha jana imepatikana, huku ikielezwa chanzo cha ajali hiyo ni ndege hiyo kugonga mlima na kingo za kreta.

Ndege hiyo ilianguka eneo la Kreta ya Mpakai Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha na sasa miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa ajili ya taratibu nyingine.

Chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo iliyokua ikitokea mkoani Kilimanjaro kuelekea eneo Seronera Serengeti, inaelezwa ni hali ya hewa kuwa mbaya.

Akizungumza jana na waandishi wa habari eneo la tukio, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Theresia Mahongo, alisema zoezi la kutafuta miili hiyo limekwenda vizuri na kwa sasa wanaendelea na taratibu nyingine kwa ajili ya kuangalia namna ya utambuzi.

“Niseme tu mpaka sasa hivi tayari miili yote imepatikana na tutaipeleka wilayani Karatu na baadae mkoani Arusha lakini pia niwashukuru wananchi wa eneo hili kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kufanikisha zoezi hili,” alisema.

Naye Naibu Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro, Dk. Maurus Msuha, alisema zoezi la kuipata miili hiyo na kuiondoa eneo hilo limefanywa na wenyeji wa eneo hilo kwa kushirikiana na askari wa hifadhi hiyo.

“Tuliomba kulala eneo hili hasa wenyeji kwa lengo la kuhakikisha miili isiliwe na wanyama ambao wanapatakana ndani ya hifadhi jambo ambalo limesaidia kuweza kuikuta  ikiwa salama,” alisema.

Akisimulia tukio hilo mmoja wa waokoaji wa miili hiyo, Leak Thomas, alisema zoezi hilo lilikuwa gumu kutokana na eneo hilo kuwa na korongo kubwa na msitu mnene.

Lunda Moleli ambaye ni miongoni mwa mashuhuda wa ajali hiyo, alisema kabla ya ndege hiyo kuanguka ilikuwa ikizunguka kwenye korongo hilo kwa muda wa nusu saa bila kuruka kwenda kwenye maeneo mengine mpaka ilipoanguka.

“Wakati tukiwa tunaendelea na shughuli zetu za kawaida tuliona ndege ikiwa angani lakini baadae kidogo tuliona umeanza kuzunguka yenyewe ikiwa kwenye eneo la korongo hilo na baadae kuanguka chini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles