Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipendekeza jina la NASAC liondolewe kwa sababu linafanana na iliyokuwa Kampuni ya Taifa ya Wakala wa Meli (NASACO) ambayo ilikuwa na historia mbaya.
Mvutano huo ulianza leo jioni katika kikao cha jioni cha bunge, baada ya bunge kukaa kama kamati ili kupitisha muswada huo ambapo Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Profesa Norman Sigalla kuzungumza chochote kuhusiana na kauli ya waziri.
Profesa Sigalla amesema jina lazima liakisi madhumuni na kwamba amesikitishwa na kitendo cha waziri kuhitimisha kwa kuweka sentensi kiwepesi wepesi badala ya kusema tunachukua jina tutaenda kushughulilikia kwa kadri tutakavyoona inafaalakini yeye amesema huko mbeleni huko.
“Hili suala liko wazi jina lazima liakisi shughuli inazofanya, wakati sisi tunaunda mamlaka ya udhibiti ni lazima neno ‘marine’ liingie vyovyote watakavyoweka wao lakini sasa unaongelea shirika la kilimo kumbe linahusika na barabara, ndiyo kitu tulicholetewa leo,” amesema.
Akitoa ufafanuzi Profesa Mbarawa amesema kamati na wabunge wameelezea wasiwasi wao na serikali imeipokea na kwa kuwa ni serikali sikivu italifanyia kazi kwa kuwa sheria siyo msahafu ikiwezekana wataibadilisha.
Kabla hajamaliza kuzungumza Spika Ndugai alisema: “Waziri kwa majibu hayo, kwa hatua hii… sijui niseme nini, kwa hatua hii ndiyo tunatunga sasa sheria kwa hiyo majibu hayo kama yaliwezekana kote huko siyo hapa sasa hapa tunaelewana, kulia, kushoto ama kati.
“Sasa sidhani kama serikali wote ninyi mko tayari kuondoka na muswada wenu huu kwa sababu tu ya jina mbona liko wazi hili jambo, jina lazima liakisi madhumuni sasa angalau mtushauri vingine, tatizo letu ni jina tu, kwamba huyu ni mkristu ana jina la kiislamu, huyu ni muislamu ana jina la kikristu tunataka akae sawa.
“Natoa muda wa saa moja kwa serikali na kamati kujadiliana ili tuufanyie maamuzi muswada huu, katika hili tuko very serious na hatutanii, kamati na serikali nendeni baada ya hapo mwenyekiti wa kamati uje utoe taarifa kisha nawahoji wabunge kuhusu muswada huu baada ya saa moja.”