30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MASHINE ED-XRF YAWA SULUHISHO KWA WAKULIMA, WACHIMBA MADINI

 

AZIZA MASOUD ALIYEKUWA MBEYA


TATIZO la uwepo wa pembejeo zisizo na ubora limekuwa changamoto kubwa kwa wakulima hasa   kwa zao la korosho  ambao kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakisumbuka.

Pamoja na jitihada za Serikali kuhakiki pembejeo  zinazoingia nchini kupitia sekta mbalimbali, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wakulima wa mikoa hiyo juu ya mada ya  uwepo  wa viuatilifu vya dawa  ya aina ya salfa visivyo na ubora.

Tatizo la kupatiwa salfa isiyo na ubora ni  ni kilio cha wakulima hasa mikoa ya kusini ambao zao lao kuu la biashara ni korosho.

Agosti mwaka huu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, aliagiza  kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya viongozi waliohusika na usafirishaji wa salfa ambayo ilikuwa mbioni kusambazwa kwa wakulima wa wilayani Tandahimba kwa madai ya kuwa imekwisha muda wake.

Agizo la Dendego alilitoa baada Taasisi ya Kuchunguza Wadudu waharibifu wa Mimea (TPRI) kuthibitisha kuwa salfa hiyo iliyokadiriwa kuwa   tani 20 iliyokuwa katika katika ghala la Naliendele mkoani Mtwara, kwenda  kwa wakulima wilayani Tandahimba kuwa  haifai kwa matumizi ya wakulima.

Ili kupunguza tatizo hilo ambalo linasababisha uharibifu wa mazao kwa wakulima, Maabara  ya Mkemia  Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imeanza  utaratibu wa kuwasaidia wakulima kupata salfa  yenye ubora  baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara  kwa kutumia mashine maalumu ya ED-XRF.

Kaimu Meneja wa Ofisi ya Mkemia  Mkuu wa Kanda hiyo ambayo inajumuisha mikoa sita ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa na Katavi, Gasper Mushi, anasema mashine ya ED-XRF ambayo imenunuliwa Oktoba mwaka jana kwa gharama ya Sh milioni 97, ilianza kufanya kazi Machi mwaka huu.

Anasema mashine hiyo  ambayo kazi yake ni kupima sampuli za mazingira pamoja na kwamba ililenga kuwasaidia zaidi wachimbaji wadogo katika  kujua kiasi   cha madini kilichopo kwenye michanga,  kwa sasa imekuwa msaada zaidi kwa wakulima wa zao la korosho.

“Hii mashine ipo moja tu katika ofisi ya Mkemia Mkuu na  imeletwa katika ofisi hii ya  kanda kutokana na uhitaji wake, huku  kuna migodi,  hivyo lengo lilikuwa ni kuwasaidia wachimbaji kujua  kiasi cha madini kilichopo  chini ya ardhi, baadaye tukagundua pia ina uwezo wa kupima ubora wa kiuatilifu cha salfa ambacho hutumika kunyunyuzia mazao ili kuua  wadudu na magonjwa ya mazao,” anasema Mushi.

Anasema huduma ya upimaji wa ubora wa salfa haitolewi kwa   mwananchi mmoja mmoja isipokuwa inafanywa  chini ya  usimamizi wa Wizara ya Kilimo pamoja na TPRI.

“Mashine hii inawasaidia sana wakulima, kulikuwa na changamoto  na  malalamiko ya wakulima kwamba wanatumia viuatilifu visivyo  na ubora hasa salfa, waingizaji wengi walikuwa wanasambaza salfa ambayo haziui wadudu, tangu walipoanza kuja kupima katika mashine yetu hii siku hizi malalamiko hayo yamepungua,” anasema Mushi.

Kwa upande wa Jansen Bilaro ambaye ni Mkemia Daraja la Pili katika ofisi hiyo, anasema salfa zisizo na ubora zilikuwa zikiingia kutoka  nje ya nchi  japokuwa kulikuwa na utaratibu wa upimaji kabla ya uwepo wa mashine hizo lakini  bado kulikuwa  na malalamiko.

“Hizi salfa nyingi  zinatoka katika nchi za Marekani, India na Chile ili iweze kuwa na ubora  na isaidie kuua wadudu, inatakiwa  iwe asilimia 98 na asilimia mbili yawe matakataka, ikiwa tofauti unaikuta salfa inakuwa asilimia 70 hiyo sasa haiwezi kufanya kazi,” anasema  Bilaro.

Anasema walipoanza kazi ya kupima Januari mpaka Machi, walikuwa wanapokea  sampuli zisizo na ubora lakini kwa sasa tatizo hili limekuwa tofauti kwakuwa waingizaji wameanza kuwa makini katika kuhakikisha kuwa na ubora unaostahili wa bidhaa hiyo.

Anasema  salfa zilizopokelewa  na kupimwa kuanzia Mei  mpaka Septemba  mwaka huu, zilikuwa na kiwango cha ubora kilichowekwa kwa ajili ya kuulia wadudu.

“Mpaka sasa tumepima sampuli za salfa zaidi ya 300, kati ya hizo asilimia 60 zilikuwa sawa na asilimia 40 zilikuwa chini ya kiwango,” anasema Bilaro.

Anasema mashine hiyo mbali na kupima salfa pia inapima sampuli za mazingira  kugundua tatizo lililopo katika maji  ama udongo pamoja na sampuli za majani.

“Aina ya sampuli za mazingira  sehemu kubwa ni maji na udongo, unaweza ukawa unaangalia uchafuzi wa mazingira na wafanyabiashara wa madini wanataka kujua kiwango cha madini kilichopo kwenye mazingira.

“Sampuli za majani huwa zinaletwa  na wapelelezi (Jeshi la Polisi) ili waweze kukamilisha madai yao kwa ajili ya kuyapeleka mahakamani, sisi huwa tunafanya uchunguzi na kuwapa majibu ya kitaalamu na vilevile baada ya kuwasilisha huwa tunathibitisha mahakamani kama tulichokichunguza ni sahihi ili taratibu za kimahakama ziweze kuendelea,” anasema Bilaro.

Anasema sampuli 200 za majani zilipokelewa na zote zilibainika kuwa  ni madawa ya kulevya aina ya bangi.

Anasema  ili kuweza kukamilisha shughuli zao,  mbali na Jeshi la Polisi  maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali  ya kanda hiyo pia inafanya kazi na Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles