Na Amina Omari, TANGA
SERIKALI imekuwa ikiendesha zoezi la upigaji chapa (alama) mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, lengo kuu likiwa ni kutambua idadi kamili ya mifugo yake.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo takwimu zinazoonyesha kuwa nchi ya Tanzania ina idadi kubwa ya mifugo, huku sekta hiyo ikiwa bado haijaweza kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi.
Kwani bado asilimia kubwa ya wafugaji wanafanya ufugaji kiholea, huku baadhi ya mazao yatokanayo na mifugo hiyo yakishindwa kuingia kwenye soko kutokana na kutokuwa na ubora.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amefanya ziara mkoani Tanga kujionea namna ambavyo zoezi la uwekaji alama linavyoendelea na kuzungumza na wafugaji pamoja na wadau wa sekta hiyo.
Anasema Tanzania ina utajiri mkubwa wa mifugo barani Afrika, kwani ni nchi ya tatu kwa utajiri wa mifugo zikifuatia nchi za Sudan na Ethiopia, lakini bado sekta hiyo haijaweza kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa.
“Kwani takwimu za kisayansi zinaonyesha kuwa, Tanzania ina mifugo takribani milioni 28, ambapo asilimia 97 ya mifugo yote hiyo ni mifugo ya asili huku idadi ndogo ikiwa ni mifugo ya kisasa,” anasema Naibu Waziri Ulega.
Uwingi wa mifugo
Amesema kuwa kukamilika kwa zoezi hilo kutaweza kutoa taswira halisi wakati huu ambapo nchi inatekeleza sera ya viwanda, kwani itasaidia kutoa mwanga wa uwekezaji mkubwa katika sekta ya mifugo.
“Tunahitaji uwekezaji wa viwanda kwa ajili ya kuchakata nyama pamoja na bidhaa zitokanazo na mifugo, hivyo ni lazima kuhakikisha tunakuwa na mifugo yenye ubora na kuwa na takwimu za uhakika,” alisema Naibu Waziri.
“Hivyo amesema kuwa iwapo hakuna hatua za haraka zitakazoweza kuchukuliwa ikiwemo kufanya udhibiti wa mifugo yetu, kwa sasa tunaweza kuimarisha mifugo ya wenzetu.
Uvamizi wa mifugo
Waziri Ulega anasema zoezi hilo litasaidia kutambua uingiaji wa mifugo kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wakiingia kwa wingi katika ardhi ya nchi yetu kwa ajili ya kutafuta malisho.
Anasemai mara nyingi ifikapo wakati wa kiangazi malisho yanapokuwa haba ndipo wafugaji huanza kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho.
“Changamoto kubwa ipo katika maeneo ya mipakani ambapo ndipo wafugaji hutumia fursa hiyo kuingiza mifugo nchini na wafugaji wa nchini
kuipeleka nje ya nchi kwa kisingizio cha kutafuta malisho,” anasema Ulega.
Licha ya mkakati huo bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maeneo ya malisho pamoja na mitamba bora kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.
Hivyo Waziri Ulega anasema kuwa ili kumaliza tatizo la malisho, Serikali inatarajia kuzirejesha ranchi zote zilizobinafsishwa kwa watu binafsi na kushindwa kuziendeleza na kuzigawa kwa wafugaji wengine.
Ranchi za malisho
Anasema lengo la kuchukua ranchi hizo ni kusaidia kumaliza changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji kugombania maeneo ya ardhi kwa ajili ya malisho na kilimo.
Hivyo, anasema Serikali imeamua kuja na mpango huo ili kuepusha wafugaji wetu hususani wale waishio mipakani kwenda kwenye malisho ya mifugo yao katika nchi jirani.
“Tutachukua mapori yote ambayo wamiliki wake wameshindwa kuyaendeleza na kuyagawa kwa wafugaji ili waachane na ufugaji wa kuhamahama ambao umekuwa hauna tija kwao,” anasema Naibu Waziri huyo.
Ameongeza kuwa utaratibu huo utakapokamilika utasaidia wafugaji hapa nchini kuweza kufuga kisasa na kuachana na kufuga kiholela ikiwemo kumaliza migogoro baina yao na wakulima.
Matumizi bora ya ardhi
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amewataka watendaji kuimarisha mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yote ili kuepuka migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
“Iwapo mtatenga maeneo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi, basi migogoro baina ya wakulima na wafugaji itaweza kuwa historia ndani ya nchi hii kwani kila mtu ataweza kufanya shughuli zake bila usumbufu,” anasema Waziri huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, akizungumzia changamoto za ufugaji mkoani humo, anasema kuwa ni pamoja na baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kupakana na hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
“Hifadhi ile imepakana na mto Mkomazi ambao ndio unategemewa na wanyama walioko hifadhini pamoja na mifugo, hivyo hapo ndipo penye changamoto ya mifugo kuchanganyika na wanyama wa hifadhi,” amesema RC
Shigela.
Anasema changamoto hiyo ya ukosefu wa malisho inachangia wafugaji wengi kukimbilia nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kutafuta maeneo ya malisho.
Mitamba
Akizungumzia changamoto ya mitamba bora, Naibu Waziri huyo anasema Serikali imejipanga kuagiza mitamba 600 kutoka nje ya nchi na kuisambaza nchini kote.
Anasema lengo la Serikali ni kuhakikisha kupitia mitamba bora itakayozalishwa na vituo vyetu vya nchini na itakayoagizwa kutoka nje kusaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa kutoka lita milioni mbili kwa mwaka hadi kufikia lita milioni 3.8 .
“Tutahakikisha wafugaji wetu wa ng’ombe wa maziwa wanafaidika na ufugaji huo kwa kuwasaidia kuongeza uzalishaji lakini pamoja na kuimarisha masoko ya ndani na nje,” amebainisha.
Anasema kupitia mpango wa ‘Tanzania Livestock Master Planning’, TLMP tunatarajia kufanya maboresho makubwa katika sekta ya mifugo na kuifanya yenye tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Uzalishaji nyasi
Ili kukabilina na changamoto ya uhaba wa malisho katika kipindi cha kiangazi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Mkoa wa Tanga, John Bwire, ameiomba Serikali kuzijengea uwezo taasisi zake za utafiti ili waweze kuja na suluhisho la changamoto hiyo.
Anasema taasisi hiyo ina uwezo wa kutafiti mbegu bora ya nyasi itakayoweza kutoa malisho mengi na mfugaji kuweza kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi ya malisho kwa kipindi cha kiangazi.
Anasema mbegu hiyo ambayo wameshaifanyia utafiti wa awali ina uwezo wa kudumu zaidi ya miaka mitano na kusaidia kuzalisha nyasi kwa wingi tofauti na nyasi za kawaida.
Naye Daktari wa Mifugo Mkoa wa Tanga, Dkt Zodiac Lyimo, anasema mkoa huo una upungufu mkubwa wa mitamba bora kwani hitaji halisi ni mitamba 1000 wakati iliyoko kwa sasa ni mitamba 200 tu.
Anasema ili kumaliza changamoto hiyo, juhudi za makusudi zinahitajika ili kuweza kumkomboa mfugaji lakini pia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa ya maziwa kutoka lita 50,000 hadi kufikia lita 120,000 kwa siku.
Wakati huo huo Serikali imecharuka kuhusu mifugo toka nchi jirani kuvamia mbuga za Taifa.
Waziri Mpina ang’aka
Serikali imekusanya zaidi ya Sh milioni 200 kutokana na ng’ombe waliouzwa kwa mnada katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuingizwa nchini isivyo halali.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, anasema wizara yake imejipanga kuendelea na operesheni maalumu ya kukamata na kuondoa mifugo yote inayoingizwa kutoka nchi jirani kupitia mikoa ya mipakani ya Katavi, Kigoma, Tanga, Mara, Ruvuma na Arusha na kuagiza wakuu wa mikoa na wilaya hizo kuendesha operesheni hizo maalumu ndani ya siku saba.
Mpina anasema Serikali haipo tayari kuingia gharama ya kutibu magonjwa yanayoletwa na mifugo inayoingizwa nchini kinyemela na kuleta uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo, kusababisha mmomonyoko wa udongo na kuchangia kwa kiasi kikubwa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi la mifugo kutoka nchi jirani kulisha mifugo yao kibabe nchini na kuvuruga mwenendo wa ujirani mwema. Serikali imepiga marufuku wafugaji kugeuza Tanzania kuwa ni nchi ya malisho ya mifugo yao.