NAIROBI, KENYA
KINARA mwenza wa muungano wa National Super Alliance (Nasa), Musalia Mudavadi juzi alisema wataitisha kura ya maoni kuibadili Katiba kuhakikisha chaguzi za haki zinafanyika.
Akizungumza katika mazishi ya mke wa aliyekuwa mpambe wa harusi yake, Mudavadi pia aliponda kitendo cha Kanisa la Katoliki kuibuka sasa kutaka kuongoza majadiliano kutatua mkwamo wa kisiasa nchini humo
Kuhusu kura ya maoni, Mudavadi alisema Nasa imeamua kutumia nguvu ya umma kama njia ya kusukuma mabadiliko ya sheria za uchaguzi.
‘Haitachukua muda tutaitisha kura ya maoni, ambapo tunalenga kuhakikisha nguvu ya umma inaonekana na kutoa funzo kuwa haipaswi kuchezewa.
“Chama cha Jubilee kimejipanga kutumia wingi wao bungeni na hili ndilo tunalojipanga kupambana nalo,” alisema.
Ametoa hatua hiyo huku kaunti nne za Siaya, Homa Bay, Busia na Vihiga tayari zimeridhia kuanzishwa kwa mabunge ya watu
Mabunge zaidi ya Kaunti hasa zilizo chini ya upinzani yanatarajia kufuata huku Kaunti ya Kakamega ikitarajia kujadili suala hilo kesho.
“Hatutambui chaguzi za Agosti 8 na Oktoba 26. Tunataka mpangilio mpya wa makubaliano, chaguzi za haki na heshima kwa kila anayepiga,” alisema wakati wa mazishi ya shemeji yake Mary Muhonja.
Muhonja ni mke wa Alfred Lulu, ambao waliokuwa wapambe wa Mudavadi wakati wa harusi yake.
Aidha Kiongozi huyo wa Chama cha Amani National Congress (ANC) alisema Kanisa la Katoliki ‘limekumbuka shuka kumekuchwa.’
Ukosoaji wake huo ulitokana na taarifa ya maskofu wa Kanisa la Katoliki kuwa wataongoza majadiliano ya kitaifa kufuatia mgawanyiko mkubwa uliosababishwa na marudio ya uchaguzi wa urais.
“Kanisa la Katoliki sasa linatoa mwito wa majadiliano. Lakini walikuwa wapi muda wote huo?’
“Tunakaribisha nia yao njema lakini wafahamu kuwa ‘walizika vichwa vyao mchangani muda wote ule,” alisema.