Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
WAMILIKI wa vyombo vya habari nchini (MOAT) wameunda kamati ndogo ambayo itakwenda Dodoma kuonana na wabunge waweze kupinga muswada wa vyombo vya habari ambao una vipengele 10 vinavyodaiwa kukandamiza uhuru wa habari nchini.
Muswada huo ambao unatarajiwa kuwasilishwa hivi karibuni una vipengele hivyo ambavyo vikipitishwa vinaweza kuwafanya wanahabari kushindwa kutimiza majukumu yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, wamiliki hao walisema kamati hiyo itakutana na Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni kujadili suala hilo.
“Pia tutakutana na wabunge wa kamati zinazohusu vyombo vya habari tuweze kuwaeleza vipengele ambavyo vinaweza kuua uhuru wa habari nchini,”alisema Mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi.
Alisema katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu, serikali inataka kuingia kwenye mgogoro na vyombo vya habari jambo ambalo linaweza kusababisha wanahabari kushindwa kutimiza majukumu yao.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo pia itakutana na wanasheria kuangalia na kuvijadili vipengele kandamizi viweze kufanyiwa marekebisho.
“Mkakati wetu ni kuhakikisha muswada huu haupiti kwa sababu haufai, umelenga kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari nchini,”alisema.
Alisema wanasiasa ni vigeugeu kwa sababu wanapokuwa wanataka kuingia madarakani wamekuwa wakiwashirikisha wanahabari katika shughuli zao lakini baada ya kupata wanawageuka na kushindwa kuwatambua waliowasaidia kufika hapo walipo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited(MCL), Fransic Nanai alisema vyama vya upinzani vimekuwa mstari wa mbele kupinga muswada huo, hivyo vinapaswa kuungana nao kuhakikisha haupiti.
“Juzi niliwasikia Chadema wakisema wataupinga muswada huu kwa vurugu bungeni hivyo basi tushirikiane nao kuhakikisha haupiti,”alisema Nanai.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sahara Media, Samuel Nyara, alisema kamati hiyo inapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo wabunge wa vyama vyote waweze kujadili kwa kina namna ambavyo muswada huo unawakandamiza wana habari.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali halisi, ambayo inamiliki gazeti la Mwanahalisi lililopo kifungoni, Saed Kubenea, alisema muswada huo umelenga kuwafunga wanahabari wasiweze kutumiza majukumu yao.
“Wametung’oa kucha, wametutoboa macho, sasa wameamua kutufunga tusiweze kutumiza majukumu yetu,”alisema Kubenea.
Vipengele vinavyolalamikiwa ni pamoja na kipengele cha kutoa adhabu za kutisha kwa makosa 10 yakiwamo ya utangazaji, uasi, uchochezi na makosa ya habari za uongo ambako mtuhumiwa atapaswa kulipa faini ya Sh milioni 20, kifungo au vyote kwa pamoja.