29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SIKUKUU ZINAKUJA, UMEJIPANGAJE?

Na ATHUMANI MOHAMED

BILA shaka mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku salama kabisa. Kwa upande wangu miye ni mzima na nipo tayari kuwaletea somo jingine wiki hii kama ilivyo ada ya safu yetu hii inayojadili mambo yahusuyo maisha.

Ndugu zangu, tupo katika kuelekea kwenye kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka. Leo ni Novemba 11, zimebaki takribani siku 18 ili kumaliza mwezi na kuingia mwezi Desemba, ambao huwa na pilikapilika nyingi.

Ni mwezi ambao wanafunzi wengi wanakuwa wamefunga shule/vyuo. Ni wakati ambao wafanyakazi wengi hupenda kuchukua likizo kwa ajili ya kupumzika na familia au kusafiri hadi kijijini kuwajulia hali ndugu na jamaa.

Ni mwezi ambao una shughuli nyingi; ubarikio, harusi, kupongezana na hata sikukuu rasmi kama Krismas na baadaye Mwaka Mpya. Kwa hakika ni wakati wa kutumia fedha zaidi kuliko kuingiza.

Ingawa kwa wenzetu wanaofanya kazi zinazohusiana na sanaa ni wakati wao wa kutengeneza fedha zaidi kwani sikukuu zote hizo huambatana na burudani ambazo hutotewa na wasanii ambao wataingiza vipato kutokana na sanaa yao.

Najua kuna watu watajiuliza; huyu Athumani vipi, mbona ameanza kuzungumzia mambo ya sikukuu mapema kiasi hiki? Jibu ni moja tu, nataka kukumbusha kupanga mambo yako mapema, ili isije mwezi Desemba ukaondoka na kukuacha ukiwa mifuko mitupu!

Tatizo Waafrika wengi hatuna utamaduni wa kupanga mambo yetu, kila kinachotokea maishani mwetu kinakuwa kama ajali tu. Hili ni kosa kubwa sana.

PANGA BAJETI YAKO

Acha kufanya mambo kwa zimamoto, sikukuu haziji kwa ghafla, zinajulikana. Kwa msingi huo basi unatakiwa kuwa na bajeti yako mapema. Epuka ile tabia ya kununua vitu kwa sababu pesa ipo mikononi mwako muda huo.

Kuishi kwa mtindo huo ni hatari, unaweza kununua vitu bila mpangilio na baadaye ukajikuta huna fedha tena. Kinachofuata hapo ni kuingia kwenye madeni ambayo yanaweza kukuharibia utaratibu mzima wa mipango yako.

ANZA NA VIPAUMBELE

Kwenye bajeti yako anza na vitu vya muhimu. Mfano una watoto watatu, ni wazi kuwa unapaswa kutenga bajeti ya nguo za watoto wako hao. Kumbuka mavazi mapya ni muhimu sana kwa watoto. Kwao ni kitu chenye thamani kubwa sana wakati wa sikukuu.

Ukishaweka hesabu za mavazi, unatakiwa kuangalia vyakula, zawadi za ndugu, safari ya utalii nk. Hiyo sasa ni kulingana na mahitaji yako kwa kadiri unavyoyajua, kuyapenda na kupanga kuyafanya.

FANYA MANUNUZI SASA

Katika kipindi cha sikukuu na hasa kuanzia juma la pili la mwezi Desemba, vitu vingi huanza kupanda bei hadi kufikia juma la tatu, bidhaa nyingi zinakuwa zimepanda bei maradufu.

Kuepuka hilo, anza kununua vitu mapema kuanzia sasa. Mfano nguo za watoto na zawadi nyingine, ni vema kununua sasa ili kupishana na mfumuko wa bei hapo baadaye. Hata baadhi ya vyakula visivyoharibika kama mchele, maharage, tambi nk, unaweza kununua mapema.

KUWA NA KIASI

Usifanye mambo kwa kufuata mkumbo, angalia kipato chako. Kuwa na kiasi katika matumizi yako. Unaweza kutumia fedha nyingi katika kipindi kifupi na ukaja kujuta baada ya sikukuu kupita.

Kamwe sikukuu isigeuke matatizo kwako. Panga na timiza yale yaliyo ndani ya uwezo wako. Usikubali kujiumiza, ufahari wa siku moja unaweza kugeuka mateso kwako kwa kipindi kirefu.

Muhimu na la mwisho ninakuacha nalo ni kwamba, siku zijazo ujenge utaratibu wa kuandaa mambo yako mapema kabla siku husika haijafika. Ndugu zangu ni vizuri kufanya mambo yako kwa ratiba na siyo kushtukiza.

Nawatakia mema katika kuyatimiza hayo. Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles