Na JANETH MUSHI -ARUSHA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imewahukumu wafanyakazi sita wa Benki ya Exim tawi la Arusha kifungo cha jumla ya miaka 27 kutokana na mashitaka 318, ikiwamo utakatishaji fedha haramu.
Pia mahakama hiyo imewaachia huru watuhumiwa wengine saba ambao hawakukutwa na hatia, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kutoa ushahidi uliothibitisha makosa hayo kutendeka.
Watuhumiwa waliokutwa na hatia ni Lilian Mgeye, Daud Nhosha, Dorothy Chijana, Genes Masawe, Christopher Lyimo na Deusdetith Chacha.
Akisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya saa nne jana, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Desderi Kamugisha, alisema mshitakiwa Mgeye alikutwa na hatia katika makosa 10 ya utakatishaji fedha haramu na adhabu ya kila kosa ni miaka mitano, pia adhabu ya kila kosa katika makosa 12 ya kughushi nyaraka za benki ni miaka minne.
Pia alisema Nhosha alikuwa na hatia katika kosa moja la kughushi nyaraka za benki na adhabu yake ni tofauti, kwa kuwa kifungo cha juu ni kifungo cha maisha, ila anampunguzia na kumpa cha miaka minne.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Felix Kwetukia na washitakiwa waliwakilishwa na mawakili Adam Jabir, Mosses Mahuna na Philip Mushi na Hakimu Kamugisha alisema Chijana alikutwa na hatia katika makosa 18 ya kughushi nyaraka za benki na alihukumiwa miaka minne, huku Masawe na Lyimo wakihukumiwa miaka minne kila mmoja baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya kughushi nyaraka za benki.
Alisema Chacha alikutwa na hatia katika makosa matano ya kughushi na kuharibu nyaraka na megine matano ya utakatishaji fedha haramu.
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili juu ya adhabu kwa washitakiwa na kwa kuwa ni mara yao ya kwanza kutenda kosa katika shitaka la utakatishaji fedha haramu, nimeangalia vitu vingi hivyo adhabu zote zitaenda kwa pamoja,” alisema na kuongeza:
“Mgeye anahukumiwa miaka mitano, Nhosha miaka minne, Chijana miaka mitano, Masawe miaka minne, Lymo miaka minne kwa sababu adhabu zote zinaenda pamoja.”
Awali mawakili wa utetezi waliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu washitakiwa hao kutokana na kutenda makosa hayo kwa mara ya kwanza.
Baada ya hukumu hiyo, Wakili Mallya aliwasilisha kwa njia ya mdomo kusudio la kukata rufaa kwa washitakiwa hao waliokutwa na hatia.
Washitakiwa hao walikabiliwa na mashitaka tofauti, ikiwamo kughushi nyaraka, kuharibu nyaraka na wizi wa zaidi Sh bilioni saba katika benki hiyo na upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 37 na upande wa utetezi ulikuwa nao 17.
Pia Jamhuri walikuwa na vielelezo 20, ikiwamo risiti za benki za malipo ya wateja wa kampuni mbalimbali za kitalii zilizokuwa zikilipwa katika benki hiyo kwa ajili ya wageni wa nje waliokuwa wakienda katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), vocha na nyaraka nyingine ziliwasilishwa.
Katika kesi hiyo namba 309 ya mwaka 2013, watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2011 na 2013, huku washitakiwa wawili, Joyce Kimaro na Mosses Aloyce, walishaachiwa na mahakama hiyo baada ya kukiri kosa na kulipa faini.