33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MOHAMMED DEWJI APONGEZA JITIHADA ZA RAIS MAGUFULI KUFUFUA VIWANDA

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji, amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, Dewji alitoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa Global Business Forum 2017 (GBF) kuhusu viwanda kwa nchi za Afrika uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Mfanyabiashara huyo ambaye anatajwa kumiliki viwanda 41, alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati.

Dewji alisema kampuni yake ya MeTL Group itaendelea kushirikiana na Serikali na katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo amejipanga kuhakikisha anatoa ajira kwa Watanzania 100,000 jambo ambalo linadaiwa litasaidia kukuza uchumi wa nchi na kwa wananchi.

“Nianze kwa kumpongeza Rais John Magufuli, kwa shabaha yake ya viwanda, ni nzuri sababu kuna ongezeko la thamani lakini pia watu wanaweza kupata ajira na pia hizi biashara zitalipa kodi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja nchini, aliongeza kuwa utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo anategemea kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo uchumi wa Tanzania utakuwa umekuwa sana.

Pia, Dewji alizungumzia umuhimu wa mkutano wa GBF ambao umekutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wakiwepo viongozi wa Serikali za nchi za Afrika na wawekezaji, alisema ni nafasi ya kipekee kwani pamoja na kujadili viwanda pia amepata nafasi ya kuwaelezea washiriki wa mkutano fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.

“Umuhimu ni mkubwa sana, nakuja hapa kama Mo, lakini pia nawakilisha nchi yangu Tanzania, nimeitangaza nchi yangu ili watu waje na wawekeze, nimewaeleza mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tuna malighafi na tunahitaji viwanda angalau watu wetu wa Tanzania wapate ajira na Serikali ipate kodi,” aliongeza Dewji.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles