PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA
UPELELEZI wa kesi ya utakatishaji fedha wa Dola za Marekani milioni 6 inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili bado haujakamilika ikiwa ni mwaka mmoja na nusu sasa.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na Mwanasheria Mkuu wa Stanbic, Sioi Solomon.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, alieleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa, kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Wakili Mutalemwa alidai kuwa bado wanasubiri awamu ya pili ya upelelezi kutoka nchini Uingereza na kuiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo.
Hata hivyo, Hakimu Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 10, 2017 kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 1, 2016, wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015, wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.
Pia wanadaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam, walijipatia Dola za Marekani milioni 6, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.