NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
ALIYEKUWAÂ Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliyeshtakiwa kwa kupokea rushwa ya Sh milioni 323 za Escrow kutoka kwa James Rugemalira ameachiwa huru.
Mujunangoma ameachiwa huru jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, baada ya Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai kuomba kesi hiyo iondolewe mahakamani hapo.
Swai aliwasilisha hoja hiyo kutokana na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuondoa keshi hiyo chini ya kifungu namba 98 (a) cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), akieleza kuwa hana sababu za kuendelea na kesi hiyo.
Rugonzibwa alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 14,2015 Â Takukuru akikabiliwa na shtaka la kupokea rushwa ya Sh milioni 323 kutoka kwa James Rugemalira fedha ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Esrow.
Mshtakiwa huyo aliwahi kubadilishiwa mashtaka na kusomewa hati mpya ya mashtaka ambapo haikuonesha tena kuwa fedha alizopokea Mujunangoma zilitoka kwa Rugemalira na ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kupitia hati hiyo mpya, Rugonzibwa alikuwa akidaiwa kuwa Februari 5, 2014 akiwa mtumishi wa Serikali kama Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake namba 00120102602001 iliyopo Benki ya Mkombozi .
Alidaiwa kuwa alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
Ilidaiwa baada ya kujipatia kiasi hicho cha fedha alishindwa kueleza maslahi yake kwa Katibu Mkuu wa wizara yake ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi.
Awali alipofikishwa mahakamani na kusomewa hati ya kwanza alikuwa akidaiwa kuwa Februari 5, 2014 katika Benki ya Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard Rugemalira kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo fedha ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.