25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI: KINA KENYATTA BADO WACHUNGUZWA ICC

HAGUE, UHOLANZI

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), bado inachunguza ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya, ambazo awali zilishuhudia Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto na mwanahabari Joshua arap Sang wakishtakiwa.

Hayo yalibainika katika ripoti ya mwaka 2016/2017 iliyowasilishwa na Rais wa ICC, Jaji Silvia Fernandez de Gurmendi kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) juzi, huku kesi dhidi ya washtakiwa wakuu zikiwa zimefutwa.

Ripoti hiyo ilisema: “Ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka iliendelea kupokea taarifa kuhusu madai ya uhalifu dhidi ya ubinadamu uliotendeka wakati wa ghasia za 2007-2008 na kuzuru nchi mbili kuhusu uchunguzi huo.”

Kesi ya Rais Kenyatta, Ruto na Sang ambaye alikuwa mtangazaji wa redio, zilikuwa za mwisho kusitishwa katika mahakama hiyo.

Kiongozi wa Mashtaka, Fatou Bensouda, aliamua kuzisitisha kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha kuthibitisha iwapo washtakiwa hao walihusika na tuhuma zilizotolewa dhidi yao.

Alilalamika kutoweka kwa mashahidi wakuu na kudai wengine walihongwa na baadhi kuuawa, huku pia akilalamika Serikali ya Kenya kutotoa ushirikiano kumsaidia kukusanya ushahidi aliohitaji.

Hata hivyo, mahakama ilitoa agizo la kukamatwa kwa Walter Barasa, Paul Gicheru na Philip Kipkoech wanaodaiwa kuhusika katika njama za kushawishi mashahidi wajiondoe katika kesi hizo.

Watatu hao wanatakiwa mahakamani kujibu mashitaka kwa mujibu wa Ibara ya 70 ya Mkataba wa Roma, ambayo inahusu uhalifu dhidi ya utendaji wa haki.

“Uchunguzi unaendelea kuhusu madai ya uhalifu dhidi ya utendaji haki,” ilisema ripoti ya ICC.

Katika hotuba yake, Jaji Gurmendi alisisitiza kuhusu hitaji la mataifa kushirikiana na mahakama hiyo ili ifanikishe majukumu yake, hasa inapohitaji washukiwa wakamatwe.

“Mahakama hii iliundwa kwa imani kuwa aina hizi za uhalifu husababisha tishio kwa amani na usalama. Kwamba upelelezi na kufungua mashtaka kutasaidia kuzuia uhalifu zaidi na kuchangia kudumisha amani. Kwa kufanya hivyo, mahakama hailengi mataifa wala kanda fulani bali kulinda waathiriwa wa uhalifu,” alisema.

Aliongeza kuwa mahakama hiyo imeweka mikakati ya kuimarisha uadilifu wa wafanyakazi wake na kufanya marekebisho ya sheria zake.

Katika wiki chache zilizopita, uadilifu wa maofisa wa ICC ulitiliwa shaka baada ya madai kuibuka, kwamba aliyekuwa Kiongozi wa Mashtaka, Louis Moreno Ocampo, alisaidia baadhi ya washukiwa kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles