NA ESTHER MBUSSI
ASKOFU Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, amesema kwa sasa nchi bado ni changa hali inayoondoa utayari wa kuongozwa na mtu anayenyoa ‘unga’ (kipara).
Mbali ya kusema nchi haiko tayari kuongozwa na wanyoa unga, pia alisema wakati wa Tanzania kuongozwa na vijana haujafika.
Kauli hiyo ya Dk. Mokiwa imekuja siku chache baada ya Mbunge wa Bumbuli, January Makamba kutangaza nia ya kuwania urais na kudai kuwa ni wakati wa vijana kushika hatamu ya madaraka.
Makamba ambaye ni mmoja wa makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioadhibiwa kutokana na kuanza harakati za kuwania kiti cha urais kabla ya wakati, alitangaza nia yake hiyo alipofanya mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza (BBC) Idhaa ya Kiswahili, ambapo mbali ya kusema amejitathmini na kujiona anafaa, pia alisema huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola.
Katika kuhakikisha anaboresha nia yake, Makamba alivitaja vipaumbele vyake pindi chama chake kitakapompa nafasi ya kuwania nafasi hiyo kuwa ni ajira, huduma za jamii, uchumi imara na utawala bora
Hatua hiyo ya Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imeibua mjadala mpya wa uzee na ujana, ambapo wanasiasa, wasomi na watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakijadili hoja hiyo kwa mapana na marefu, huku baadhi yao wakimuunga mkono na wengine kumpinga.
Dk. Mokiwa ambaye ni mmoja wa viongozi wa dini wanaoheshimika nchini, ameonesha dhahiri kutokubaliana na hoja ya kijana kuongoza nchi kwa sasa, ambapo aliweka wazi kuwa muda wa vijana kuongoza nchi haujafika.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili kuhusu suala la rais ajaye, Dk. Mokiwa alisema Tanzania ni taifa changa ambalo linahitaji kuongozwa na mtu aliyekomaa kimawazo na maono ya kutosha.
Akizungumzia hatua ya Makamba kutangaza nia, Dk. Mokiwa alisema kama kweli mwanasiasa huyo kijana anataka kugombea urais anapaswa kujitengeneza kwa namna ambavyo taifa linamtaka awe si kwa sababu baba yake alikuwa na cheo.
“Nafasi hiyo inataka mapafu yaliyokomaa, huko nyuma tuliona baadhi ya vijana walioingia kwenye nafasi za juu ambao ilibidi kuwasimamia ili kwenda sawa.
“Sifa za urais si suti, urais ni taasisi pana, kwanza hatujawahi kuwa na kiongozi anayenyoa unga, kama anataka kutuongoza inabidi ajiangalie mwenendo wake mara mbili zaidi,” alisema Dk. Mokiwa.
Alipoulizwa suala la kunyoa kipara linahusiana nini na urais na hasa ukizingatia wapo baadhi ya viongozi kama vile, Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye ananyoa kipara, alisema kwa Zuma huo ni utamaduni wa kabila lao la Kizulu na kwamba kwa Tanzania si sahihi.
Hata hivyo, Dk. Mokiwa alisema kama Makamba anaona umri unamruhusu kugombea nafasi ya urais na kama havunji sheria za chama chake katika kutangaza nia kabla ya wakati hakuna tatizo, lakini alimtaka kutumia nafasi hiyo vizuri.
“Nchi hii tuna kiu ya kupata kiongozi bora, tunapenda tupate kiongozi ambaye amekomaa, atakayeiletea nchi amani.
“Mtu anayejua kuongoza nchi maskini na yenye amani, atakayepunguza wimbi la viongozi kutibiwa nje ya nchi kama Afrika Kusini, India na kwingineko,” alisema Dk. Mokiwa.
Aidha, Dk. Mokiwa alihoji karipio la Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) lilikuwa mahususi kwa ajili ya nani kwani Makamba ni mmoja wa wanasiasa walioadhibiwa na chama hicho kutokana na kuanza kampeni mapema.
“Nakumbuka karipio hilo lilikataza watu kusema nataka urais, sasa huyu amesema lakini hakuna hata katazo lililotolewa dhidi yake, je, hii inamaanisha chama chao kimetoa ruhusa kwa wengine huku wengine wakikatazwa,” alihoji Dk. Mokiwa.