Na ELIYA MBONEA – ARUSHA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala, amesema Serikali inakusudia kusitisha utoaji wa leseni kwa Kampuni ya uwindaji ya Otterlo Business Corporation (OBC).
OBC iliyoanza uwindaji mwaka 1992 baada ya kupewa leseni na Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Abubakar Mgumia, imekuwa ikiendesha shughuli hizo kwenye pori tengefu la Loliondo lililopo katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Akizungumza wilayani hapa juzi, wakati wa majumuisho ya ziara yake, Kigwangala, alisema uamuzi huo unatokana na kampuni hiyo kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, kuwa na migogoro isiyoisha na wananchi, hususani jamii ya wafugaji wa Kimaasi.
Waziri Kigwangala alisema OBC haitakuwa sehemu ya kampuni za uwindaji zitakazopewa upya leseni ya uwindaji hapo mwakani, hiyo ni kutokana na kuwapo kwa madai ya uvunjifu wa haki za binadamu, ikiwamo kujihusisha katika migogoro eneo hilo kwa zaidi ya miaka 25.
Alisema kampuni hiyo haitapatiwa tena leseni mpya mwakani, kutokana na kuwa na mkono katika migogoro inayoendelea kwenye eneo hilo la pori tengefu la Loliondo.
“OBC ipo nyuma ya vurugu hizi, siku zao zinahesabika, hawatapewa leseni mpya ya uwindaji Januari mwakani,” alisema Waziri Kigwangala.
Aidha akiwa Loliondo katika ziara yake, Kigwangala aliagiza mifugo yote iliyokuwa ikishilikiwa na bado wamiliki wake hawajafikishwa mahakamani, iachiwe mara moja wakati mazungumzo kwa pande zote yakiwa yanaendelea.
Pia aliagiza wafugaji walioondolewa mifugo yao katika pori hilo, ikiwamo pia maeneo ya mipakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, waanze kunyweshea mifugo yao katika mito iliyomo ndani ya pori tengefu la Loliondo.
Akiwa mkoani Dodoma hivi karibuni, Kigwangala alisitisha leseni zote za uwindaji katika vitalu na kutaka utaratibu mpya wa kununua vitalu hivyo ufanyike kwa mtindo wa mnada.
Akizungumza na wadau wa utalii na uhifadhi, alisema kwamba hatua hiyo inalenga kulinufaisha zaidi taifa kutokana na rasilimali zilizopo.
Katika mkutano huo, Kigwangala aliwaambia wadau hao kwamba ni Tanzania pekee katika nchi zilizopo Kusini mwa Sahara ambayo imekuwa haikodishi vitalu vyake vya uwindaji kwa kutumia mnada.