GENEVA, USWISI
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetengua uamuzi wake wa awali wa kumteua Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe kuwa Balozi Mwema wa chombo hicho barani Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alituma ujumbe wa tweeter ambao uliwekwa katika tovuti ya WHO, ikiufahamisha umma uamuzi wao.
Katika taarifa hiyo, Dk. Ghebreyesus alisema alisikia mlolongo wa shutuma dhidi ya uamuzi huo na kuamua baada ya kuzungumza na Serikali ya Zimbabwe kwamba ni kwa maslahi ya WHO kutengua uamuzi huo.
Taarifa yake katika tovuti ya WHO ilisomeka: “Kipindi cha siku chache zilizopita, nimekuwa nikifikiria kuhusu uteuzi huu wa Mheshimiwa Rais Robert Mugabe kuingia WHO kuwa Balozi. Kwa sababu hiyo, nimeamua kutengua uteuzi huo.
‘Nimesikiliza kwa makini wale walioeleza wasiwasi wao na kusikiliza masuala tofauti waliyoibua. Nimeshauriana pia na Serikali ya Zimbabwe na kufikia uamuzi kwa maslahi ya WHO,” alisema.
Awali Serikali ya Uingereza ilisema, imeshtushwa na kuvunjika moyo kuwa WHO imemtaja Mugabe kuwa balozi wa nia njema.
Msemaji wa serikali hiyo mjini London, alieleza kuwa Mugabe anakabiliwa na vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) na hivyo kitendo cha kumteua kitaathiri kazi za WHO.
Awali akifafanua uamuzi wa uteuzi huo, Dk. Ghebreyesus, alisifu namna Zimbabwe inavyozingatia afya ya umma.
Lakini wakosoaji wanasema katika kipindi cha miaka 37 ya utawala wa Mugabe, huduma za afya zimekuwa mbaya huku wahudumu wa afya wakiwa hawalipwi mara kwa mara na kumekuwa na ukosefu mkubwa wa dawa muhimu.
Dk. Tedros, raia wa Ethiopia, ambaye ni Mwafrika wa kwanza kuongoza WHO na alichaguliwa kwa ajili ya kukabiliana na kile kilichoaminika kugeuzwa kwa shirika hilo kuwa la kisiasa.