Na ASHA BANI
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi namba 52 ya kupinga kuvuliwa uaskofu iliyofunguliwa mwaka huu na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa.
Kesi hiyo iliwasilishwa Mahakama Kuu Tanzania dhidi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, kupinga uamuzi wa Rita wa kumwondoa katika orodha ya wadhamini baada ya Januari 7, mwaka huu, kuvuliwa uaskofu na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Jacob Chimeledya, kutokana na tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya uaskofu na katiba ya Kanisa hilo.
Katika kesi hiyo, Serikali iliwakilishwa na Wakili Benjamin Mihayo na Mokiwa aliwakilishwa na Wakili Ally Hamza na Wakili Lukoma.
Jaji wa Mahakama Kuu, Isaya Halfani, alisema mahakama imeona kuwa kesi ya Mokiwa imefunguliwa kinyume cha sheria kutokana na sababu moja kati ya nyinginezo, kwamba maombi yaliletwa mahakamani kwa kutumia vifungu vya sheria visivyo sahihi.
Pia mahakama hiyo imemwamuru Mokiwa kulipa gharama za kesi hiyo.
Kabla ya kesi hiyo, Mokiwa aliwahi kufungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kutetea nafasi yake, lakini iliondolewa kwa kukosa uhalali mahakamani.
Mawakili wa upande wa utetezi katika kesi hiyo walidai kuwa, kesi hiyo ilihusu masuala ya kiroho na haikustahili kwa mlalamikaji kuipeleka mahakamani.