Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Serikali kurekebisha sheria ya kanuni ya adhabu na ya ugaidi inayotoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi.
Pia kituo hicho kimempongeza Rais John Magufuli kwa kueleza bayana kwamba hatatekeleza adhabu ya kifo.
Septemba 12 mwaka huu, wakati akimwapisha Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Rais Magufuli alisema hana mpango wa kunyonga watu hivyo asipelekewe orodha ya waliohukumiwa adhabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, alisema adhabu ya kifo inakiuka haki ya msingi ya binadamu kuishi na kuondoa uwezekano wa mkosaji kujirekebisha, na badala yake inaendeleza ukatili dhidi ya ubinadamu.
LHRC imezitaka mamlaka husika kuweka adhabu mbadala wa kifungo cha maisha ili kuthamini uhai ambao ni haki ya kila binadamu.
Aliitaka Serikali kutekeleza pendekezo la mpango wa kujitathimini wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2016, kwa kuridhia mkataba wa nyongeza wa haki za raia na siasa na kutangaza kuwa haitekelezi adhabu hiyo.
Alisema Tanzania inapaswa kujifunza kutoka kwa mataifa mengine duniani ambayo hayatekelezi adhabu ya kifo.
Henga alisema badala yake hutoa adhabu mbadala kama vile kifungo cha maisha na kazi ngumu kwa watuhumiwa wa mauaji ili kulinda haki ya msingi ya kuishi.
“Kama watetezi wa haki za binadamu tunampongeza Rais Magufuli kwa kuweka wazi msimamo wake wa kutounga mkono adhabu ya kifo,”alisema Henga.
Alisema LHRC inapinga kuondolewa adhabu hiyo kwa sababu ni ya ukatili na isiyo na staha, inayotoa utu wa binadamu na inayofanya Serikali ionekane ni mhalifu kwa kuua.
“Hii ni adhabu ya ubaguzi maana mara nyingi wanaopatikana na hatia na kupewa adhabu ni masikini wasioweza kuwa na uwakilishi na ushauri wa sheria,”alisema Henga.
Alisema adhabu ya kifo inavunja misingi ya tamko la kimataifa la haki za binadamu la mwaka 1948 ambalo linaeleza kuwa kila mtu ana haki ya kuishi.
Alisema hadi sasa hakuna ushahidi kuwa kuwapo adhabu hiyo unasaidia kupunguza uhalifu badala yake mauaji yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2016, takwimu zinaonyesha hadi mwaka 2015 kulikuwa na watu 472 waliohukumiwa kunyongwa, kati yao wanaume wakiwa 452 na wanawake 20.
Pia, kati ya hao wanaosubiri kunyongwa ni 228, huku 244 wakisubiri uamuzi wa rufaa zao.
Alisema taarifa ya haki za binadamu ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na watu 472 wanaume wakiwa 452 na wanawake 20, ambao walihukumiwa kunyongwa, kati yao 228 wanasubiri kunyongwa na wengine 224 wanasubiri uamuzi wa rufaa zao.
“Licha ya adhabu hii kutotekelezwa nchini tangu mwaka 1994, Mahakama imeendelea kutoa hukumu hii ya kinyama na isiyokubalika kwa wote wanaoheshimu haki za binadamu na utu wa mtu,” alisema.
Alisema kutokana na mfumo wa sheria nchini kuwa na mianya mingi ya makosa ni vigumu kuwa na uhakika kuwa haki itatendeka wakati wa upelelezi, ubambikwaji kesi, changamoto za upelelezi na waendesha mashtaka kuweza kufanya makosa.
“Tunapenda kuweka wazi kwamba hatukubaliani na vitendo vyovyote vya mauaji na kwa namna hiyo hiyo tusingependa kuona muuaji anauawa baada ya kuua, kufanya hivyo ni kuhalalisha kifo, kukubaliana na wauaji na kuondoa kabisa utu wa mtu.
“Serikali itekeleze pendekezo la mpango wa kujitathimini wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2016 kwa kuridhia mkataba wa nyongeza wa haki za raia na siasa na kutangaza rasmi kuwa haitekelezi adhabu ya kifo,” alisema.