33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

WASIOLIPIA HATIMILIKI KUPOTEZA MAENEO YAO

NA CLARA MATIMO – MWANZA

SERIKALI  kupitia Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, imetahadharisha wananchi kuwa watapoteza haki ya kumiliki viwanja vyao endapo watashindwa kulipia malipo ya kuandaliwa hatimiliki.

Angalizo hilo lilitolewa na Ofisa Mipango Miji wa Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza, Kenedy Chiguru, juzi baada ya kuona wananchi  hawajalipia gharama za kuandaliwa hati wakidhani kwamba gharama walizotoa kupimiwa maeneo yao ndizo zitakazotumika kuandaliwa hatimiliki.

Akizungumza na  MTANZANIA ofisini kwake, alisema urasimishaji makazi katika baadhi ya mitaa iliyopo ndani ya  kata 15 wilayani humo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, la Oktoba 12, mwaka jana akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.

Chiguru alisema Waziri Lukuvi aliagiza ukamilishaji wa upimaji wa viwanja 35,019, kati ya hivyo Halmashauri ya Ilemela viwanja 16,141 na Nyamagana 1,8878.

“Urasimishaji makazi ulikuwa na mwitikio mkubwa wakati wa upimaji, wananchi wengi walijitokeza na kulipia gharama za kupimiwa maeneo yao, lakini baada ya kuona vigingi vimepandwa kwenye viwanja vyao wanadhani ndiyo mwisho wa zoezi.

“Dhana hiyo ni potofu kwa sababu ili utambulike kisheria na uwe na uhakika pia usalama wa kiwanja chako ni hadi pale utakapokuwa na hatimiliki ya kiwanja hicho.

“Wananchi wengi bado hawajajitokeza kulipia gharama za maandalizi ya hatimiliki wakati zoezi linaenda kufikia ukomo Oktoba 15, mwaka huu,” alisema Chiguru.

Aidha, Ofisa huyo wa Mipango Miji alisema  Jiji la Mwanza limeandaliwa Mpango Kabambe (Master Plan) ulioanza mwaka 2015 hadi 2035, uzinduzi wake utakapofanyika umilikishaji wa viwanja utafanyika kwa kuzingatia matumizi yaliyowekwa na mpango huo tu na si vinginevyo, huku akiwataka wananchi watumie fursa hiyo mapema kabla zoezi halijafikia mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles