NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu(CCM) ameitaka jamii kuacha kulijadili kwa mtazamo wa siasa, suala la matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu (Chadema), anayetibiwa Nairobi, Kenya kwa kuwa kufanya hivyo kutachangia kuligawa Taifa.
Nyalandu alitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na Kituo cha Star Tv alipokuwa akizungumzia masuala mbalimbali, hasa ushiriki wake katika matibabu ya Lissu.
Alisema kitendo cha mtu kuhusika na kumshambulia kwa risasi Lissu, lilikuwa jambo la kushtusha na liligusa mioyo ya watu wengi.
“Jambo la kumsaidia Lissu limeelezwa vizuri, kwa kuangalia utashi wa familia, Serikali na wana Chadema kila mtu anajaribu kuangalia maslahi mapana ya afya ya Lissu.
“Kamwe tusilichukulie suala la Lissu kisiasa, matibabu ni dhamana ya chama hiki au kile, mimi nasema tuwe na fursa za kutofautiana kwa hoja, kuumwa si suala la siasa,”alisema Nyalandu.
Alisema tukio hilo linapaswa kulaaniwa kwa kuwa kama limeweza kumtokea Lissu pia linaweza kumtokea mtu mwingine.
“Niwakumbushe tu mimi naingia hapa katika matibabu kama jirani, yule ni kaka yangu, mbunge mwenzangu wa Singida kuona jambo hili lililofanyika limetugusa kiasi gani,”alisema Nyalandu.
Nyalandu ambaye anadai alilia baada ya kupata taarifa hizo, alisema ameamua kuungana na watu wanaomsaidia Lissu kwa kuwa anahitaji mkono wa ukombozi ili apone.
Alisema tukio hilo ambalo limefanywa na watu wabaya wa mbunge huyo, linapaswa kulaaniwa na kila Mtanzania kama alivyofanya Rais Dk.John Magufuli na viongozi wengine wa Serikali, vyama na dini.
“Ni muhimu kufahamu tundelee kulaani kwa sababu linagawa Taifa na kuleta mmomonyoko … limenisikitisha kwa sababu mimi mbunge wa CCM napakana na Lissu,”alisema Nyalandu.
Alisema kinacholeta ustawi wa jamii ni kuwa na mijadala ya wazi, kutofautiana kwa mawazo kwa wazi na kushindana kwa hoja na si vingine.
“Naamini jambo hili la Lissu linawaunganisha sana watanzania isipokuwa katika mazungumzo kwa kuwa huwezi kuwazuia watu kuongea.
“Wana midomo, wapo wanaotaka kulionyesha kwamba lipo tofauti, nawaona watu wachache kuliko watanzania na viongozi wengi kutoka chama cha CCM na viongozi wachache,”alisema Nyalandu.
Alisema mbunge huyo amepona kwa miujiza kwa kuwa mara kadhaa amekwenda kumtembelea Nairobi na aliona hali yake haikuwa nzuri.
“Nilipoenda mara ya kwanza ilitangazwa lakini nimeenda tena mara kadhaa ambazo sijaziripoti, nimeona ile hali lakini ninaamini kwamba Mungu amemfanya Tundu Lissu kuwa miujiza.
“Nimeona miujiza mingi lakini kilichomtokea Lissu, Mungu aliruhusu aishi kwa kuwa Mungu amemfanya aishi, hili jambo tuliamishe liwe la taifa lisitugawe,”alisema Lazaro.
Alisema watanzania waguswe na kilichompata mbunge huyo na siyo kugeuza maneno na matendo yao kwa kutumia utashi wa ndani ya mioyo yao.
Alisema bila kujali tofauti zozote za siasa, kabila na itikadi watanzania wanapaswa kuungana kumuombea.
“Kwa sababu madaktari wanaomtibu ni watu, wakikosea sehemu moja anaweza akapata shida zaidi, tumuombe Mungu azidishe fahamu za wale wanaomtibu arudi katika hali yake ya kawaida,”alisema Nyalandu.
Alisema anaiona safari ndefu ya matibabu ya Lissu hasa kipindi hiki cha kumuweka sawa katika majeraha aliyoyapata.
“Mtu ukiumia sana sehemu za mwili hata ukiungwa kwenye mifupa,sehemu za ndani, kuna mambo mengi ambayo hatuyajui yatatokea hivyo atahitaji muendelezo wa mazoezi ya mwili na viungo, na ushauri wa saikolojia,”alisema Nyalandu .
Alisema ushauri wa saikolojia utamsaidia kufahamu kwamba kilichotokea kilikuwa na nia mbaya kwake lakini Mungu alikuwa na nia nzuri zaidi.
Nyalandu alisema amekuwa akisaidiana na Chadema kuhakikisha unafanyika utaratibu wa kumpeleka nje ya nchi kuhakikisha anapatiwa matibabu zaidi.
Alisema ili kukamilisha mpango huo anaendelea kufanya mazungumzo na marafiki zake walioko Ulaya na Marekani.
Mbunge huyo alisema amekwisha kufanya mazungumzo na hospitali ambayo itakuwa tayari kumsaidia pamoja na madakatari wake.
Alisema kinachoendelea sasa ni kufuata ushauri wa madaktari wa Nairobi ambao walimzuia kutokana na hali yake.
Kuhusu uvumi wa kufukuzwa CCM, Nyalandu alisema kitu hicho hakipo wala hajawahi kupatiwa barua ya onyo tangu alipojiunga na chama hicho.
“Saa nyingine siyo kila lisemwalo lazima ujibu, tangu niwe mwanachama sijawahi hata kupatiwa barua ya onyo.
“Nilichaguliwa awali mwaka 2005 nikiwa mbunge mdogo zaidi, sasa nipo mara ya nne. Naamini katika kujadiliana masuala ya wazi na ukweli ni kwamba maswali magumu katika jamii hayana majibu rahisi,” alisema Nyalandu.