Na PETER FABIAN- MWANZA
GARI dogo la abiria la Toyota Hiace lililokuwa linatoka Buhongwa kwenda Kivuko cha Kigongo wilayani Misungwi mkoani Mwanza, limetumbukia ndani ya Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 12, wakiwamo dereva na kondakta wake.
Taarifa kutoka eneo la tukio zilisema ajali hiyo ilitokea jana saa 6:50 mchana baada ya mfumo wa breki za gari hiyo namba T 229 BBW kushindwa kufanya kazi.
Katika eneo tukio, miili tisa ya watu wazima na watoto watatu iliopolewa majini huku majeruhi watatu wakipelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Bukumbi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, kwa matibabu.
Mashuhuda wa ajali hiyo walilieleza MTANZANIA jana kuwa gari hilo linalofanya safari zake kati ya Buhongwa na Kivuko cha Kigongo kilichopo Kata ya Idetemya wilayani Misungwi lilitumbukia ndani ya Ziwa Victoria kwenye kivuko hicho.
Mashuhuda hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walieleza kuwa kabla gari hilo halijafika kivukoni umbali wa mita 200, abiria mmoja mwanamke aliomba ashushwe kutokana na mwendokasi wa gari.
Baada ya abiria huyo kushuka gari liliendelea na safari kuelekea kivukoni huku likiwa kwenye mwendokasi.
Walisema kabla ya kutumbukia majini liligonga vizuizi vya kivuko na kupita katikati ya magari yaliyokuwa yakisubiri kuvushwa na feri na kutumbukia ziwani.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda akizungumza kwa simu alieleza kuwa wakati ajali hiyo inatokea alikuwa kwenye ziara vijijini.
Alisema baada ya kupata taarifa alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi kwenda eneo la tukio na yeye akakatisha ziara yake.
Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga aliliambia gazeti hili kwa simu kwamba alipokea taarifa hizo kwa mshituko na masikitiko makubwa ikizingatiwa idadi hiyo kubwa ya watu 12 waliofariki dunia.
“Tukio hili kwa ujumla limenisikitisha sana, hapa najiandaa kusafiri kwa ndege nirudi jimboni kuungana na wananchi waliopoteza ndugu na jamaa zao,” alisema.
Kitwanga alisema ajali hiyo iwe fundisho kwa watu wote wanaotumia vyombo vya moto huku akisisitiza kuwa polisi hawana budi wafanye uchunguzi wa kina na hatua zichukuliwe kwa waliosababisha ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akizungumza kutoka eneo la ajali, alisema chanzo cha ajali ni gari kukosa mwelekeo na kutumbukia ziwani.
Mongella alisema hatua ya kutafuta miili ilikuwa inafanywa na wazamiaji kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.
Hadi tunakwenda mtamboni, miili 12 ilikuwa imeopolewa majini na majeruhi watatu wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Misheni Bukumbi.
Kamanda
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema majeruhi watatu waliweza kutambulika, mmoja akiwa mwanamke, Sophia Mliyambina na wanaume wawili, Paul Lazaro na Yohana Ngabula.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni watoto watatu, mmoja akiwa wa kiume, Salim Msafiri mwenye umri wa miezi minane na wa kike wawili, mmoja akiwa ametambuliwa kwa jina la Pendo Msafiri na watu wazima tisa, wanawake watatu na wanaume sita.
Akizungumza na MTANZANIA hospitalini hapo, Sophia alisema alikuwa akitokea msibani nyumbani kwao Magu akiwa na watoto wake wawili, mmoja wa miaka minane na mwingine alikuwa na wiki mbili. Wote wamefariki dunia kwenye ajali.
Alisema baada ya gari kuzama alihangaika kwenye maji na kujikuta akiwa hospitalini huku akisikia maumivu makali ya kichwa na baridi kali.
Majeruhi mwingine, Mwalimu Paul Lazaro, alisema kabla hawajafikia lango la kivukoni, breki za gari zilikata.
Alisema abiria walipiga kelele na wakimwambia dereva aligongeshe gari hilo sehemu yoyote hata kwenye nyumba ili wapone lakini hakuwasikiliza.
“Baada ya gari kutumbukia ziwani mimi nilipita dirishani nikaanza kutapatapa majini, waokoaji wakiniambia nikazane kuogelea ili nijiokoe na wakanitupia kamba.
“Nilirudishwa na mawimbi nikawa nazama chini na kurudi juu… mwokoaji akaja na boya akaniambia nilishike nikafanya hivyo na kamba ya boya akaitupa nchi kavu wakaanza kuivuta na kufanikiwa kuniokoa,” alisema Lazaro.
Naye Yohana Ngabula, alisema gari hiyo ilikuwa na abiria zaidi ya 25.
Alisema alikwenda jijini Mwanza akiwa na mama yake na mdogo wake wa mwisho kwa ajili ya kufuatilia mirathi ambayo walipewa Sh milioni nne.
Ngabula alisema wakati wakiwa wanarudi Chato ndipo ajali hiyo ilipotokea ambako alimpoteza mama yake na mdogo wake.