KWAZULU-NATAL, AFRIKA KUSINI
MFALME wa Zulu, Goodwill Zwelithini, amesema kuondolewa kwa adhabu ya kiboko shuleni, imechangia kuwepo utovu wa nidhamu katika taasisi za masomo.
Alitoa matamshi hayo juzi Jumanne kwenye mkutano na walimu wakuu wa shule na wasimamizi, uliofanyika huko Kaskazini mwa KwaZulu-Natal.
Mfalme Zwelithini ambaye pia ni kinara wa elimu eneo hilo, alisema kuwa adhabu ya kiboko ilichangia wanafunzi kufanya vyema.
“Hiki kitu cha kutowaadhibu watoto wetu kimetuletea madhara kwa sababu watoto hawana nidhamu,” alisema.
Adhabu ya kiboko shuleni nchini Afrika Kusini ilipigwa marufuku mwaka 1997 japo inaendelea kwenye shule nyingine zinazokiuka sheria hiyo.
Mwezi uliopita, video ya mwalimu akimchapa viboko mwanafunzi ilisambaa kwa kiasi kikubwa katika mitandao ya kijamii, huku mamlaka ziliahidi kumchukulia hatua kali mwalimu huyo.
Pia, mfalme amelaani kuuliwa kwa kupigwa risasi mwalimu kwenye Mkoa wa Guateng, ambao ni kitovu cha uchumi wa Afrika Kusini.