NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
ULAJI wa nyama zilizonona, nyama za kuku na unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi huchangia ongezeko la mafuta kwa wingi na uzito mkubwa kwenye mwili wa binadamu, imeelezwa.
Pamoja na hayo, matumizi kupita kiasi ya mafuta ya nazi, mawese na yale yatokanayo na wanyama yanaweza kukuweka kwenye hatari ya kupata magonjwa mbalimbali, hasa ya moyo.
Hayo yalielezwa jana na Mtaalamu wa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Louiza Shem, alipozungumza na wananchi waliojitokeza kupima afya ya moyo katika taasisi hiyo, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani.
“Kwa bahati nzuri hamna chakula ambacho mtu hatakiwi kutumia ili kujiepusha na magonjwa ya moyo, lakini tunashauri jinsi gani na kwa kiasi gani uvitumie ili kuepuka kupata magonjwa.
“Mfano ukiangalia vyakula vya wanga (ugali, wali viazi na vinginevyo) unakuta mtu anakula kupita kiasi, anajaza sahani… wakati mtu anapaswa kula chakula kulingana na aina yake ya kazi anayoifanya,” alisema.
Aliongeza: “Wengi tunaofanya kazi ofisini hatutumii nguvu nyingi kulinganisha na wale wanaobeba mizigo, wengi tunakula nyama kwa kiwango kikubwa, ni vema kupunguza kiasi.
“Mafuta yanayopatikana kwenye nyama yanaongeza uzito kupita kiasi na huenda kuziba mishipa ya damu, ikiwa ni ya kichwani utapooza mwili na ikiwa ni kwenye moyo utapata ‘heart attack’,” alibainisha.
Alishauri pia jamii kupunguza kiwango cha chumvi, kwani inapotumika kwa kiwango kikubwa huathiri afya ya moyo.
“Kundi kubwa tunaloona linaathirika na magonjwa haya ni wale waliopo kwenye umri wa uzalishaji na umri unavyozidi kuongezeka ndivyo uwezekano wa mtu kupata ugonjwa huu unavyoongezeka,” alisema.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Tulizo Sanga, alisema tafiti zinaonesha kila mwaka watu wapatao milioni 17 wanafariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
“Aidha, zaidi ya watu milioni 75 kila mwaka hugundulika kuwa na ugonjwa huu, hali inaonekana kuwa mbaya zaidi katika nchi zinazoendelea,” alisema Dk Sanga, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma Bora za Afya wa Taasisi hiyo.