NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
SERIKALI imelifungia gazeti la kila wiki la Raia Mwema kwa muda wa siku 90.
Adhabu hiyo imetolewa ikiwa ni siku 10 baada ya gazeti jingine la kila wiki la Mwanahalisi kufungiwa kwa kipindi cha miezi 24 (miaka miwili) kwa kile kilichosemwa na Serikali kuwa ni mfululizo wa kukikiuka maadili, misingi ya sheria ya taaluma za uandishi wa habari, kuandika habari za uongo, uchochezi na kuhatarisha Usalama wa Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, gazeti hilo limefungiwa kutokana na kuchapisha habari ya uchambuzi yenye kichwa cha habari kilichosema ‘Urais utamshinda John Magufuli’.
Pia taarifa hiyo ilisema agizo la kusitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo linahusu toleo la mitandaoni.
Alisema Serikali imechukua uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika kifungu cha 59 cha sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016.
Alisema habari hiyo ilikuwa imesheheni nukuu zenye nia mbaya, za uongo na kutunga zinazomsingizia Rais Dk. John Magufuli.
“Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti hili kwa siku 90 kutokana na habari iliyotoka toleo namba 529 iliyokuwa na nukuu za uongo na kutungwa na zenye nia mbaya zikidai rais alipata kusema: “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji baadaye, na watakaobaki Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kweli kweli,” alisema.
Abbas alisema baada ya kuandika habari hiyo wahariri wa Raia Mwema waliitwa ili kuthibitisha nukuu hizo zilipatwa kuongelewa wapi na Magufuli lakini waliomba muda kwa ajili ya kutafuta uthibitisho wakapewa lakini walishindwa kuthibitisha na walikiri na kuomba radhi.
Alisema gazeti hilo lililopatwa kuonywa siku za nyuma kwa makosa tofauti wahariri wake waliporejea kwa ajili ya uthibisho wa nukuu hizo walisema kuwa hawana ushahidi huo na kukiri kosa pamoja na kuomba radhi.
“Serikali imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa kuwa wahariri wa gazeti hili hawakufanya tashititi na wamekiri kosa,” alisema.
Abbas alisema Serikali inaamini Watanzania wakiufanyia mzaha upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) amani na utulivu inayojivunia kwa miaka mingi vitapotea na kukaribisha maafa kama ilivyotokea kwingineko duniani.
Kwa upande wao, uongozi wa gazeti hilo umelalamikia uamuzi wa Serikali kutoa adhabu hiyo na kudai ni kubwa ukilinganisha na kosa lenyewe.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mhariri Mkuu wa Raia Mwema, Godfrey Dilunga, alisema taarifa ya kusitishiwa uchapishaji huo wameipata jana kupitia barua iliyotolewa na Abbas.
“Adhabu tuliyopewa ni kubwa kwetu, mara nyingi inapotokea tumeandika habari ambayo inaonekana ipo tofauti huwa wanatuita tunakaa tunaeleweshana na mambo mengine yanaendelea,” alisema.
Dilunga alipoulizwa kama walishawahi kupewa barua ya onyo alisema hawezi kuongelea suala hilo kwa kuwa angepaswa kutoa maelezo mengi kwa wakati huo.
Alisema jana uongozi wa gazeti hilo umelazimika kukutana na kufanya kikao cha dharura ili kujadili suala hilo.