WAKULIMA wa tumbaku mkoani Katavi, wametishia kuacha kulima zao hilo kutokana na kutolipwa fedha zao za mauzo ya msimu huu wa tumbaku.
Hatua hiyo imekuja baada ya kampuni za ununuzi wa zao hilo msimu huu kushindwa kununua tumbaku kutoka kwa wakulima kwa madai vyama vya msingi vimezalisha ziada kubwa ya zao hilo .
Wakizungumza na Mtanzania Digital, baadhi ya wakulima hao wamedai hawaoni sababu ya msingi ya kuendelea kuzalisha ziada ya zao hilo la biashara msimu ujao wa kilimo ambao unaanza Septemba kwa kuotesha mbegu kwa sababu hawajalipwa fedha zao za msimu uliopita huku tumbaku nyingine ikiwa imelundikana kwenye ghala na nyumba za wakulima.
“Tunadai fedha za msimu uliopita lakini pia tumbaku nyingine haijanunuliwa haijanunuliwa na Kampuni ya ununuzi ya TLTC kwa kile kinachodaiwa uzalishaji umezidi malengo waliyokubaliana baina ya Chama cha Ushirika na Kampuni ya TLTC, tumepoteza kabisa matumaini ya kulima tena msimu ujao,” amesema mmoja wa wakulima hao.
Meneja wa Chama cha Msingi Mpanda Kati, Amani Rajabu amesema: “Kuhusu malipo ya mauzo yao ya tumbaku wakulima wenyewe waliamua kwenye mkutano wao mkuu kuwa malipo yatakuwa yanafanyika baada ya masoko yote kuwa yamemalizika, hivyo kwenye chama hicho bado kuna kilo zaidi ya 500,000 hazijanunuliwa baada ya kuwa zimezidi kwenye makisio yao ya msimu wa kilimo wa 2016/2017.”
Msimu wa ununuzi wa zao hilo ulianza Mei mwaka huu na ulisitishwa Septemba baada ya kampuni zinazonunua tumbaku kusitisha kununua baada ya idadi ya kilo walizokubaliana kimkataba na vyama vya ushirika kukamilika.
Mwisho