Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
SARATANI ni mkusanyiko wa magonjwa zaidi ya 200 ambayo yanaweza kutajwa kulingana na eneo lililoathirika katika mwili ama aina ya chembe hai zilizohusika.
Ziko saratani zinazofahamika na zingine zimepata umaarufu kwa sababu ya kuwa katika eneo linaloonekana kama vile titi (saratani ya titi).
Pia kuna saratani ambazo hazina umaarufu mkubwa ingawa zinawaathiri watu wengi.
Mfano wa saratani hizo ni Kaposi ambayo kwa wanaume ni ya kwanza (asilimia 24) na kwa wanawake ni ya pili (asilimia 16).
Kaposi ni aina ya saratani inayoathiri mfumo wa kinga ya mwili lakini madhara yake huonekana kwenye ngozi na wakati mwingine mguu unaweza kuvimba na kuwa kama tende ama kuathiri viungo vya ndani.
Mtu mwenye saratani hii kwa kawaida huanza kuonyesha uvimbe katika ngozi yake nje ya mwili au kwenye kuta za sehemu zingine ndani ya mwili kama vile mdomoni, puani, kooni na kwenye mapafu.
Viuvimbe vya saratani hii ya kaposi kwa kawaida huonekana kama wenye rangi nyekundu, kahawia au zambarau ambapo mara nyingi huwa na maumivu na wakati mwingine havisababishi maumivu yoyote.
Saratani hii huathiri chembe hai za ukuta wa ndani wa mishipa ya damu. Kaposi huwa na hatua tofauti kuanzia kwenye ngozi hadi kuhusisha viungo vya ndani ya mwili.
Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu, Mkuu wa Idara ya Kinga wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa anasema saratani hiyo haikupewa kipaumbele kwa sababu inahusiana na Virusi vya Ukimwi (VVU) hivyo mgonjwa hunyanyapaliwa.
Kwa mujibu wa Dk. Kahesa, VVU vinaongeza hatari zaidi ya asilimia 80 katika saratani hiyo.
“Si kila mwenye saratani hii ana VVU lakini ugonjwa huo unaongeza kasi zaidi ya saratani ya kaposi na idadi kubwa ya waathirika wa ugonjwa huu ni wale wenye VVU,” anasema.
Dk. Kahesa anasema saratani hiyo husababishwa na kirusi kinachojulikana kwa jina la kitaalamu Human Herpes Type 8 (HHV8).
Anasema saratani hiyo ilikuwapo muda mrefu lakini ilikuwa haifahamiki kwa sababu miaka ya nyuma watu wengi waliokuwa na VVU walikuwa wakipoteza maisha kwa wingi tofauti na miaka ya sasa.
“Wanaume ndiyo wanaoongoza kuugua ugonjwa huu lakini haikupewa kipaumbele kwa sababu ina uhusiano na VVU hivyo kuna unyanyapaa. Sababu nyingine ni kwamba haiwaathiri zaidi Wazungu kwahiyo kulikuwa hakuna ‘focus’.
“Sasa hivi watu wengi wenye VVU wanaishi muda mrefu kwa sababu ya kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs) ndio maana tunaanza kuona saratani ambazo zina uhusiano naugonjwa huo,” anasema.
DALILI
Dk. Kahesa anasema dalili huanza polepole na huwa hazionekani mapema ndio maana wagonjwa wengi wamekuwa wakifika hospitali ugonjwa ukiwa umeshazidi.
“Ngozi inaweza kubadilika na kuwa kama kuna baka, wakati mwingine ngozi inakuwa ngumu na kupoteza mwelekeo na hata sura inaweza kuvimba.
“Mgonjwa pia anaweza kupata matatizo katika njia ya chakula, kuharisha, kuumwa tumbo, kushindwa kula ama kubanwa kifua.
Anasema dalili za awali za saratani ya kaposi ni mwonekano wa mabaka mekundu au zambarau juu ya ngozi, kisha mabaka hayo hukua na kutengeneza uvimbe kama vinundu na kwamba inaweza kuleta uharibifu kuanzia kwenye ngozi laini ya midomo na viungo vya ndani ya mwili.
“Wagonjwa wengi hupata dalili za kwenye ngozi na inaweza kusababisha aina mbalimbali za dalili kutegemea na kiungo gani kimeathiriwa,” anasema.
Kwa mujibu wa wataalamu, dalili zingine ni fizi kutoka damu, uvimbe katika miguu, madhara kwenye ngozi huweza kutokea hasa katika maeneo ya miguuni, kichwa na shingo. Pia vinundu ama vipele vya saratani ya kaposi huweza kuwa ya saizi ya kati ama vikubwa.
“Wakati mwingine ni vigumu kuvitambua kutokana na rangi ya ngozi ya mtu, hutokea zaidi kwenye ngozi laini kama mdomo, fizi na macho,” anasema Dk. Kahesa.
Saratani hii ikihusisha viungo vya mfumo wa chakula wakati mwingi vipele hivyo huwa havitoi dalili za kuonekana nje ya mwili, kama zikionekana basi ugonjwa unakuwa umekua na husababisha dalili zifuatazo;
Kushindwa kumeza chakula, ama chakula kushindwa kufika tumboni, kichefuchefu, kutapika na maumivu ya tumbo, kutapika damu, kuonekana kwa damu kwenye haja kubwa ama kupata choo cheusi, kuziba kwa utumbo.
MATIBABU
Matibabu ya kukinga madhara ya VVU kwa kutumia dawa za ARVs ni moja ya mbinu za kutibu saratani ya kaposi. Dawa hizo hutumika katika matibabu ya saratani hiyo isiyohusisha viungo vya ndani vya mwili.
Kama mtu ana saratani hii katika viungo vya ndani ya mwili matumizi ya dawa za kama chemotherapy huongezewa katika matibabu yake.
Pia matibabu ya mionzi, kukata vipele kwa njia ya cryotherapy, kukata vipele kwa kutumia mionzi ya Laser, upasuaji wa kukata vipele, matumizi ya dawa za saratani za vinka alkaloid, dawa za kupaka aina ya retinoids yanaweza kutumika kuongeza ubora wa maisha ya mgonjwa mwenye saratani ya kaposis ambayo imeharibu ngozi na kuondoa urembo.
TAKWIMU ZA SARATANI
Mwaka jana Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, iliona wagonjwa wapya 5,200 wanaosumbuliwa na saratani za aina mbalimbali.
“Kinamama wanaongoza kwa kuchukua asilimia 63 na shida kubwa kwao ni shingo ya kizazi,” anasema Dk. Kahesa.
Kulingana na takwimu hizo, saratani ya shingo ya kizazi ni asilimia 33, kaposi (16), matiti (13), tezi dume (2), njia ya chakula (11).
USHAURI
Wataalamu wa saratani wanasema hatari ya saratani huongezeka pindi kunapokuwa na visababishi vingi ikiwamo mfumo wa maisha, ulaji usiokuwa na mpangilio, kutofanya mazoezi, matumizi ya kemikali na ngono zembe. Hivyo, ni muhimu jamii ikachukua tahadhari.
“Watu wafanye uchunguzi mapema kuepuka kuona wagonjwa wakiwa katika hatua za mwisho.
“Saratani kwa kiasi kikubwa inatibika na huduma zimesambaa hospitali nyingi hivyo, watu wafike mapema na uzuri ni kwamba gharama nyingi zinalipiwa na serikali,” anasema Dk. Kahesa.
Mwisho.