29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU WA KATOLIKI ATOA UJUMBE MZITO

Na Mwandishi Wetu – Dr es Salaam


ASKOFU wa Kanisa Katoliki Ngara, Severin Niwemugizi, amesema kuongezeka kwa watu wanaoitwa ‘wasiojulikana’ ni tishio kubwa nchini.

Amesema pia kuwa yuko tayari kuitwa mchochezi endapo kundi la watetezi wa haki za binadamu watachukuliwa kama wachochezi.

Askofu Niwemugiza  ambaye anatoka Ngara mkoani Kagera, alisema hayo, Dar es Salaam  jana wakati akifungua mkutano wa asasi za raia  kuhusu Katiba Mpya.

 

Watu wasiojulikana  

Baada ya Askofu Niwemugizi kupewa nafasi ya kutoa neno la kufungua mkutano huo jana, alianza kwa kusema: “Sikutumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)  ila nimealikwa kama mimi kutoka kule Ngara ninakoishi, kuja kushiriki  mazungumzo haya ya  taifa ya kusukuma, kutafuta Katiba Mpya.

“Naomba niwaondoe hofu kuwa hapa sijaja kuendesha Misa Takatifu  ila ni kushiriki kama Mtanzania. Ni vizuri tukafahamiana kwa sababu siku hizi kuna watu wanaitwa ‘watu wasiojulikana’, na hii sasa inatisha kwa sababu wanaongezeka kila siku, hivyo tutafika mahali idadi kubwa ya watu Tanzania watakuwa ni ‘watu wasiojulikana’.

“Sasa kuwatambulisha hawa watu wa Mungu kwamba ni watu wasiojulikana, ina maana hawajulikani hata kwa wakuu wa nchi hii.

“Tutajishitukia viongozi wa nchi hii watakuwapo watu wasiojulikana…sifikiri kama ni jambo zuri”.

 

Katiba

Askofu Niwemugizi alisema yeye ni kiongozi wa dini na mdau wa Katiba  na hata siku Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete anapanga kuanzisha mchakato wa katiba mpya, yeye (Niwemugizi) alikuwa na Mizengo Pinda (waziri mkuu mstaafu) nyumbani kwake.

Alisema wakati akiwa nyumbani kwa Waziri Mkuu huyo Mstaafu, Kikwete alimpigia  simu Pinda wakawa wanazungumza kuhusu kuanzisha mchakato huo.

“Nikawa nawasikiliza tu pale  anajibu japo sikuwa najua anamwambia nini lakini nasikia wanavyojibizana. Nikasema hili ni jambo zuri, hatimaye mchakato ukaanza na ukaendelea.

“Pia   ni kati ya watu ambao tulipiga kelele sana kwa jinsi mchakato ulivyokuwa unakwenda, tulipiga kelele kama viongozi wa dini tukafika mahali tukaitwa watu tusio na maana  kwa sababu hatukuona kama mchakato ulikuwa unaenda vizuri sana.

“Na kwa kweli jinsi ulivyokuwa unakwenda, mimi niliomba kabisa kwamba usifanikiwe kwa wakati ule, na nashukuru kwamba jambo hilo halikupita kwa wakati ule.

“Lakini sasa nafikiri  ni muda muafaka tupate katiba mpya. Mimi naamini kwamba katiba ya nchi ndiyo dira kuu na nchi ikikosa dira nzuri itaendeshwa vibaya na Taifa litapotea.

“Kama taifa halitakua na katiba nzuri basi litapotea, mtu yeyote mwenye nia njema na nchi  lazima ahakikishe kwanza kuna dira nzuri inayoiongoza.

“Dira hiyo ni sheria mama kwa sababu mambo yote hapa yanatendeka kwa mujibu wa sheria, tusipokuwa na sheria mama iliyo nzuri  mambo mengine yote yanakwenda vibaya.

“Na yeyote anayefanya lolote ili kulielekeza taifa kwenye hali nzuri asipoongozwa na katiba nzuri, juhudi zake nzuri zinaweza kuishia hewani,” alisema.

Alisema pia kuwa  kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, alitembelewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambako pia walizungumza suala Katiba.

Alisema Kinana alimweleza mchakato wa Katiba Mpya umegawa Watanzania na kwamba anatamani kuona kabla ya kura ya maoni ya katiba pendekezwa, kunakuwa na mwafaka wa Katiba.

“Nikamwambia nakuunga mkono kwa asilimia 200 kwa sababu mimi hapa naitwa asiyependa Bunge la Katiba, adui wa serikali kwa sababu tu napinga mchakato wa Katiba.

“Na hii ni kwas ababu ya mambo niliyosema nikiwa Iringa kwenye sherehe ya Askofu wetu mmoja, nikasema tu kwamba, ‘kama Bunge la Katiba litachakachua ule mchakato wa Katiba, mimi nitapiga kelele kuhamasisha Watanzania tuikataa Katiba inayopendekezwa’.

“Basi tangu hapo ikaonekana haka ka bwana ni kapinzani, wakasema huyu ni Chadema na kadhalika, lakini nikasema sema unachosema lakini mimi ni kiongozi wa dini naongozwa na imani yangu na maadili kutafuta ukweli na haki.

“Basi tukaachana na Kinana, nikawa nasubiri baada ya serikali mpya kuingia madarakani.

“Kwa sababu katibu wa chama alishakuwa na tamaa ya kufikia muafaka, nikawa na tamaa ya kusikia kama tunaanza upya kupata Katiba, tumekaa kimya, Rais ameligusia lakini ikaonekana siyo kipaumbele,”alisema Niwemugizi.

Rais Magufuli.

Alisema anaamini Rais ana nia nzuri na taifa tangu awali alipoanza kupambana na rushwa, ukosefu wa nidhamu na maadili katika utumishi wa umma, kuondoa watumishi hewa, kuziba mianya ya rushwa, kulinda rasilmali za nchi ili raia wa Tanzania wanufaike na rasilimali za nchi.

Alisema   mapambano hayo ya kutaka  maskini watoke katika hali zao mbaya na wapate huduma nzuri za  jamii, yalifanya kila mtu aone dalili za matumaini ya maisha bora ya Tanzania.

“Hata hivyo naamini juhudi zake hizo na kwa wale wote tunaotaka mabadiliko chanya yakitokea katika nchi yetu ili yawe endelevu na mguso mzuri, ni lazima hizo juhudi zilindwe na Katiba nzuri ambayo itatokana na wananchi wenyewe kwa sababu ni suala la wananchi wanataka wajiongozeje,” alisema.

Alisema wananchi wanatakiwa kusema wanataka watumikeje kujiendeleza katika nchi yao, hivyo  ni wao ndiyo wanatakiwa waweke msingi wa Katiba nzuri.

Matukio ya mauaji

Alisema:  “Yale tunayoshuhudia yakitokea kwa sasa katika jamii yetu, na hata kwa majirani zetu, haya tunayosikia siku hizi…utekaji wa watoto, watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha, migogoro baina ya wakulima na wafugaji isiyoisha, mauaji ya watu wasio na hatia…

“Majaribio sasa tunayoyasikia wenzetu sasa wameanza kujaribu kugeuza vipengele vya Katiba kuwawezesha wale walioko madarakani waendelee kubaki.  Hapa kwetu limeshasikika hilo kwamba kuwe na mabadiliko ya vipengele kwa visingizio mbalimbali.

“Hizi siyo dalili nzuri kwa taifa lenye afya njema,  ni vielelezo vya dira mbaya kwa maoni yangu, kwa hiyo ni muhim kama taifa sasa tuzungumze jinsi tunavyoweza kuitengeneza dira nzuri.

“Katiba nzuri na iliyo madhubuti ambayo haitaruhusu kuchezewa na yeyote mwenye kutafuta maslahi binafsi, ni lazima tuzungumze sasa  na kudai sasa, tuipate hiyo dira nzuri”.

Yuko tayari kuwa mchochezi

Alisema yeye kama kiongozi wa dini, kitabu anachokipenda ni biblia  ambayo katika Methali, 11:14, inasema; “pasipo mashauri taifa huanguka, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu”.

“Mbele yangu hapa siamini kwamba ni genge la watu wasiojulikana, ni watu wachochezi, tuchochechee nini? Watu tunataka kuishi kwa amani kwa furaha, kwa nini tuchochee mambo mabaya?

“Mimi nafikiri hapa ni wachochezi wa maendeleo, wachochezi wa hali nzuri ya maisha mazuri ya Watanzania, na mimi haitakuwa haki kabisa kukiona kikundi hiki kikizungumzia haki za binadamu na kuitwa wachochezi.

“Kama kitakuwa kikundi cha wachochezi na askofu wa Ngara yupo tayari kuitwa mchochezi, lakini pia kitabu hichohicho (Biblia) tunasoma kwamba, ‘ni utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali ni utukufu wa mfalme kufanya uchunguzi jambo’.

“Mungu ametuficha mambo mengi sana na ni kwa utukufu wake, ametuficha mimi na wewe tusijue ni lini tutakufa na tutakufa namna gani, ni kwa utukufu wake kabisa.

“Lakini ni kwa utukufu wa mfalme kuchunguza jambo, mimi napenda kumshauri Rais wangu achunguze haya yatakayozungumzwa siku ya leo.

“Yatakayozungumzwa na hadhara hii, na nimuombe aone kwamba yana nia njema na ayafanyie kazi,” alisema na kuongeza:

“Tusimdhikaki Mungu na kubaki tunasema,’ tunampenda, tunamcha Mungu’kama hatuheshimu misingi ya ukweli, haki na utu wa binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu,” alisema.

Nyalandu

Wakati huohuo, Mbunge wa  Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, kwenye ukurasa wake wa Twitter, aliandika: “TZ (Tanzania) inahitaji Katiba Mpya, mihimili ya utawala iwekewe mipaka iliyo wazi, na kuwapo checks and balance (udhibiti) kwa Serikali, Bunge na Mahakama.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles