27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Odinga aisimamisha Kenya

Raila Odinga
Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga

NAIROBI, Kenya

HATIMAYE Muungano wa Upinzani nchini Kenya wa Mageuzi na Demokrasia (CORD), jana umesimamisha shughuli za kawaida baada ya kuitisha mikutano mikubwa ya hadhara maarufu kama Sabasaba nchi nzima.

Katika mkutano huo, Muungano ulitangaza maamuzi zaidi ya 10 ambayo Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inapaswa kuyafanyia kazi.

Muungano huo unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, chini ya vuguvugu jipya waliloliita ‘Okoa Kenya’, umetishia kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta iwapo madai yao hayatatekelezwa.

Miongoni mwa hatua hizo ni kususia bidhaa zinazouzwa kwa bei ya juu pamoja na kampuni zinazozizalisha au kuzisambaza.

Pia umetaka kurudishwa nyumbani mara moja kwa majeshi ya Kenya yaliyopo nchini Somalia, ili kuimarisha usalama wa ndani.

Kabla ya ushirika huo kusoma maazimo hayo, viongozi wakuu, maseneta na magavana wa muungano huo walipata nafasi ya kuzungumza, huku wakiipiga vijembe serikali.

Katika moja ya vijembe hivyo, kiongozi wa Muungano, Raila Odinga, alisikika akisema: “Polisi wamejazana hapa kila mahali kana kwamba kuna shughuli za kitaifa, badala ya kwenda kuimarisha usalama Mto Tana. Tunawaambia wazi kuwa Wakenya wako nyuma yetu na wala hatuhofii bunduki.”

Alisema kitendo cha Serikali ya Kenyatta kukataa kukaa nao meza moja ya majadiliano hakina maana kwamba wao wana njaa.

“Je, sisi kweli ni watu wa kwenda kunywa chai Ikulu? Ina maana hatuna chai katika nyumba zetu wenyewe?” Odinga alihoji.

“Suala la majadiliano niliuambia utawala wa Rais Uhuru kuwa kulikuwa na njia ya kutatua matatizo yanayotukabili Wakenya. Ya kwanza ilikuwa kupitia majadiliano. Uhuru awali alikubali, lakini wakati tukijiandaa kwa majadiliano, wakasema kuwa hakuna haja ya majadiliano.

“Majadiliano hayawezi tena kufanya kazi. Tuna njia nyingine ‘Okoa Kenya’ na tutatoa maelekezo zaidi kuhusu hilo, narudia tena hatuogopi bunduki na tuko tayari kuwalinda watu,” Raila alisema.

“Hakutakuwa na majadiliano zaidi kwa sababu Serikali haiko tayari kusikiliza. Tutaoanisha njia za kufuata,” alisema kiongozi mwingine wa Muungano huo, Kalonzo Musyoka na kuongeza:

“Tunataka majeshi yetu yarudi nyumbani kutoka Somalia, ambayo ndiyo inayoweza kutuhakikishia amani katika taifa letu.”

Kiongozi mwingine, Moses Wetangula, ambaye ni Seneta wa Bungoma alisema: “Mwisho wa siku tutajua wapi tulipo na wapi tunakoelekea kama nchi”.

Kila viongozi hao na wengine wa kaunti na maeneo mbalimbali waliposimama kutambulishwa na kusalimia, umati ulipaza sauti za kuipinga Serikali na kumalizia “Uhuru lazima ang’oke.”

Seneta Otieno Kajwang aliuliza: “Yuko wapi Gavana wa Nairobi? Yuko wapi Evans Kidero”. Umati ukapaza sauti: “Kidero lazima ang’oke!” Gavana Kidero anatoka Muungano unaotawala wa Jubilee.

Awali Odinga, Musyoka na Moses Wetangula ambao waliwasili eneo la tukio saa 8:58 mchana, walicheza muziki wakiwa katika sare nyeupe na kushangiliwa kwa nguvu.

Baada ya hotuba mbalimbali, maseneta Bonny Khalwale na Omar Hassan walisoma maamuzi ya Muungano huo yakiwa katika waraka kurasa nne uliosainiwa na Odinga, Kalonzo na Wetangula.

Sehemu ya waraka wenye maamuzi hayo ulisomeka:

“Sisi watu wa Kenya tumekusanyika hapa Uhuru Park katika siku hii ya kihistoria, ambayo tunaadhimisha harakati zetu za uhuru, demokrasia na utawala bora;

“Tukio hili linatukumbusha matukio ya miaka ya 1960, ambayo misingi ya demokrasia katika Katiba ya Lancaster wakati wa utawala wa marehemu Jomo Kenyatta ilikiukwa.

“Mwelekeo huo unaonekana kukumbatiwa na utawala wa huu wa Jubilee, ukilenga kuvuruga mafanikio ya kidemokrasia yaliyokwishapatikana katika katiba yetu mpya.”

“Tunashuhudia uhuru wa habari ukikiukwa kupitia sheria mpya kandamizi kwa vyombo vya habari, marekebisho hasi ya Tume ya Taifa ya Utumishi ya Jeshi la Polisi,”

“Sheria za ardhi zinazoondoa madaraka kutoka Tume ya Taifa ya Ardhi kwenda mhimili wa utendaji, marekebisho mabaya ya sheria ya Tume ya Ukweli wa Haki na Maridhiano, kuanzishwa kwa sheria inayolenga kuua vuguvugu la asasi za kiraia nchini.

“Kutokana na sababu hizo na mapungufu ya kiusalama nchini na kwamba Ibara ya kwanza ya Katiba ya Kenya inatoa madaraka yote kwa watu wa Kenya. Huu ni wakati wa kuchukua hatua.”

Kutokana na sababu hizo na nyingine, Muungano wa Cord umeamua kuanzisha vuguvugu la wananchi la Okoa Kenya.

“Vuguvugu hili la watu limelenga kusaidiana katika nyakati nzuri na mbaya, kulinda kulinda mafanikio yaliyopatikana katika utawala wa kidemokrasia, na kwa ajili ya umoja, amani na usalama wa kitaifa.

“Tunautaka utawala wa Jubilee kushughulikia kupanda kwa gharama za maisha kwa kupitia upya mfumo wa kodi.”

Cord ilionya kwamba kushindwa kufanya hivyo kutawafanya wasusie matumizi ya bidhaa na huduma ambazo wananchi wa kawaida hawawezi kustahimili bei zao.

Mbali ya kuzisusia, limetishia kuweka vikwazo kwa kampuni zitakazopuuza madai halali ya wananchi wa Kenya.

Cord pia imetaka kuanzishwa kwa Kamati ya Taifa ya Kura ya Maoni (NRC), ikiwa na madhumuni ya kuwaandaa watu wa Kenya kushiriki kura mbalimbali za maoni za taifa kuhusu changamoto kali zinazolikabili taifa.

Aidha wametaka NRC ipewe mamlaka ya kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kura za maoni kwa ngazi zote za Kaunti, Tarafa na Kata kote nchini Kenya.

“Kwa vile tumepoteza imani na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC); sasa tunataka kuvunjwa mara moja na kuanzishwa kwa chombo kipya cha uchaguzi.

“Tunataka kumalizwa mara moja kwa vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya fedha, ukopaji wa kiholela ndani ya Serikali ya Jubilee.”

Katika hilo, Cord imeutaka utawala wa Jubilee ufute mikataba yote ya kifisadi, ikiwamo ule wa ununuzi wa kamera za usalama, ambao umekabidhiwa kwa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom.

Pia Safaricom ijitoe katika mikataba yote ambayo imedai imeipata isivyo halali, badala yake iwanie mikataba kwa njia ya ushindani.

Iwapo hilo halitatekelezwa, Cord imeazimia kuwahamasisha Wakenya kuweka vikwazo dhidi ya Safaricom na kampuni nyingine zinazojihusisha na rushwa au ukiritimba kama Safaricom.

Cord pia imeutaka utawala wa Jubilee uchukue mara moja hatua za makusudi za kuwaondoa askari wa Kenya kutoka Somalia ili kurudi kuimarisha usalama wa nyumbani.

Katika hilo pia wameitaka Serikali ya Jubilee ichukue hatua za makusudi kushughulika na hali ya ukosefu wa usalama, ikiwamo kuwawajibisha maofisa waandamizi wa usalama kwa mauaji na ulemavu wa mamia ya Wakenya wasio na hatia waliopata katika mashambulizi na migogoro mbalimbali kote nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles