28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Warioba: Ujana si sifa za urais

NA FREDY AZZAH, DAR ES SALAAM:

Jaji Joseph Warioba
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema uzee na ujana siyo sifa za mtu anayestahili kuwa Rais wa Tanzania atakayepatikana baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Warioba aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na gazeti hili kufafanua habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA), ikimkariri akisema rais ajaye anapaswa kuwa kijana.

Akifafanua, Warioba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema ameshangazwa na namna suala la uzee na ujana lilivyogeuzwa na kufanywa kuwa sifa mama ya mtu anayepaswa kuwa rais ajaye kinyume na kile alichokizungumza wakati akihojiwa na gazeti hilo.

Jaji Warioba alisema anaamini jambo lililosababisha kukuzwa kwa ajenda hiyo ya uzee na ujana kwa sasa ni kukithiri kwa makundi ya urais.

“Umefika wakati sasa Watanzania wafikirie sifa za mtu anayefaa kuwa kiongozi bora, badala ya kuendelea na ajenda ya uzee na ujana. “Niliwaambia (waliokuwa wananiuliza maswali) kwa nini sisi tuliokwishastaafu tuingizwe huko (kwenye kugombea urais), wananchi wapo wanaona nani anafaa, siyo kwenda na kuwaambia. Wao wanaona, tukazanie sifa za mtu anayefaa kuongoza,” alisema Warioba.

Alisema kauli yake wakati alipozungumzia suala hilo ilitokana na swali aliloulizwa kuwa yeye pamoja na Dk. Salim Ahmed Salim wamekuwa wakitajwa na baadhi ya watu na kuwaomba wawanie nafasi hiyo.

“Nashangaa kwanini hili suala liwe issue, najua yote ni kwa sababu ya makundi, kauli yangu ilitokana na swali nililoulizwa kuwa kumekuwa na watu wakitufuata na kuniomba mimi na Dk. Salim tugombee. Nikasema nini kimelikumba taifa hili mpaka sisi tuliokwisha ng’atuka tugombee tena, kwa hiyo hoja ilikuwa ni sisi personal (binafsi),” alisema.

Akizungumzia urais, alisema ni vyema sasa Watanzania wakafikiria sifa za mtu anayefaa kuwa kiongozi bora, badala ya kuendelea na ajenda ya uzee na ujana. Katika siku za karibuni kumekuwapo na makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo yamekuwa na msuguano mkali hadi kufikia hatua ya makada wake kupewa onyo kali.

Alipoulizwa ni athari gani anazoziona kutokana na makundi hayo, Warioba alisema; “Hakuna jipya, nimekwisha sema sana lakini kwa sasa haya mambo ya siasa naomba mtuache.”

Jaji Warioba alisema sifa za kuwa kiongozi alishazisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995.

Katika hotuba ambayo Mwalimu aliitoa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM waliokuwa wamekutana katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma mwaka 1995 kuchagua mgombea wa urais, alitaja sifa za mtu anayefaa kuwa kiongozi bora ambazo mpaka leo zimekuwa zikitumiwa na wanasiasa na watu wa kada mbalimbali kupima viongozi wao.

Mwalimu alitaja sifa nne kuu za kiongozi aliyekuwa akimtaka, moja ikiwa ni mtu ambaye angeweza kupambana na rushwa, ya pili ilikuwa ni kumpata mtu aliyekuwa anafahamu nchi ya Tanzania bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi ambao bado ni masikini. Sifa ya tatu aliyoitaja Mwalimu Nyerere ni mtu ambaye angepambana na udini pamoja na ukabila.

Suala la vijana kugombea nafasi ya urais na kutaka umri wa kuwania nafasi hiyo upunguzwe, lilianza kupigiwa chapuo na baadhi ya wabunge kuanzia mapema mwaka 2012.

Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, walikuwa mstari wa mbele kutaka umri huo upunguzwe kutoka miaka 41 sasa hadi 35.

Hoja hiyo iliingizwa hata wakati wa mchakato wa kuandikwa Katiba mpya, lakini Tume ya Jaji Warioba haikuingiza suala hilo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo kwa sasa inajadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Wakati wa vuguvugu hilo la kupigia chapuo hoja hiyo, wakizungumza kwenye Kongamano la Katiba na Vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Femina HIP, Dar es Salaam, Zitto na Makamba pia walitaka umri wa kupiga kura uanzie miaka 16 badala ya 18.

Akichangia hoja, Makamba alisema ili kugombea urais katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, raia husika anatakiwa kuwa na umri wa miaka 35. “Hatutakuwa tumeanza sisi kwa sababu nchi nyingi duniani nafasi ya urais inagombewa kuanzia miaka 35, kwa hiyo vijana tuangalie suala hilo katika mchakato wa Katiba Mpya inayokuja,” alisema.

Makamba alisema Katiba Mpya inayokuja iwawezeshe vijana kupiga kura wakiwa na umri wa miaka 16 badala ya 18: “Umri wa kuanzia miaka 16 unatosha kabisa kuchanganua ni kiongozi wa aina gani anafaa kuchaguliwa.”

Kauli ya Makamba iliungwa mkono na Zitto, ambaye alizitaja nchi za Kenya, Uganda na Burundi kuwa urais unagombewa kuanzia miaka 35. Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles