Na ASHA BANI, MWANZA
WAHENGA walisema; “samaki mkunje angali mbichi.” Huu ni msamiati ambao unafananishwa na mtoto katika kumjenga kitabia tangu akiwa mdogo hadi anapokuwa mkubwa.
Mtoto anatakiwa kupewa malezi mazuri na elimu ili kumjengea msingi imara katika maisha yake. Ni muhimu kila mtoto kupata elimu kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, hii itamsaidia kumudu maisha na kuepuka utegemezi.
Serikali katika kuhakikisha kila mtoto anakwenda shule, si kwenda tu bali pia kupata elimu iliyobora kwa maisha yake ya usoni, imekuwa ikibuni njia mbalimbali za kumuwezesha kupata elimu, mojawapo ni kutoa elimu bila malipo.
Ili kuunga mkono jitihada za Serikali, jamii nayo inapaswa kuweka msisitizo katika suala zima la elimu, kuwasomesha watoto wakiwa katika umri mdogo yaani kuwa na msingi wa elimu ya awali.
Elimu ya awali humsaidia mtoto kujifunza na kuwa na uelewa mpana pindi anapojiunga na darasa la kwanza.
Hivyo basi, mwanzoni mwa Februari 2014, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda alizindua Programu za Kitaifa za Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) ‘KKK’.
Mpango huo ulikuwa wa miaka mitatu ambao unalenga kuwasaidia wanafunzi walio na umri kati ya miaka 5-13 unaolenga kuwafikia watoto walio katika mfumo rasmi na wale walio kwenye vituo vya elimu nje ya mfumo huo.
Programu ya LANES imefanikiwa hasa katika Jiji la Mwanza kwani watoto wameonesha kuwa na uelewa wa haraka katika eneo mahususi la Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, wakati anazindua taarifa za wanafunzi za mpango wa KKK anasema umeonesha mafanikio kwa kiasi kikubwa kwa mwaka jana ukilinganisha na wakati ulipoanza mwaka 2014.
Profesa Ndalichako anasema kulifanyika utafiti wa mpango huo mwaka 2016, katika shule za msingi 650 na wanafunzi 7,000 walifanyiwa majaribio na kubainika kuwa wanaweza.
MPANGO WA KKK
MTANZANIA lilifanikiwa kuzunguka katika shule zilizopo mkoani Mwanza kuangalia utekelezaji wa programu ya KKK.
Lilizunguka katika baadhi ya shule ikiwamo Shule ya Msingi ya Samia iliyopo Wilaya ya Nyamagana. Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Salama Hussein anasema mpango wa KKK umesaidia kuwafanya wanafunzi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu wakiwa katika umri mdogo.
Anasema tangu Serikali kuanzisha mpango huu, walikabidhiwa vitabu vya kutosha na vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa walimu.
Vifaa hivyo vimewasaidia kufundisha na asilimia kubwa ya watoto wanaelewa vema ambapo namba ya wasiojua kusoma ni chache ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“Awali kulikuwa na watoto wengi wasiojua kusoma, kuandika, na kuhesabu lakini tangu progamu ya KKK inazishwe imesaidia kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi kukutana na mwanafunzi wa shule ya msingi ambaye hajui KKK ni nadra mno,” anasema Mwalimu Hussein.
Anasema shuleni kwake darasa la kwanza wapo 295 ambao wanasimamiwa na walimu waliopatiwa mafunzo ya kufundisha KKK chini ya mradi wa LANES utakaohitimishwa Desemba mwakani.
Anasema kuwa changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni uhaba wa madarasa, ambapo Serikali kupitia halmashauri imekuwa ikifanya kila linalowezekana kumaliza tatizo hilo.
Anataja idadi ya wanafunzi shuleni hapo kuwa ni 1,338 huku madarasa yakiwa nane yenye wanafunzi kuanzia awali hadi darasa la saba.
Anasema awali darasa moja lilikuwa wakikaa wanafunzi 300 lakini tangu serikali ianze kuboresha miundombinu ya shule na kuongeza madarasa, sasa hivi darasa moja wanakaa wanafunzi 180.
Anasema mpango wa KKK shuleni hapo unafanikiwa kwa sababu unashirikisha jamii kupitia kamati za shule kusisitiza wazazi kuwaandikisha watoto kuanza na elimu ya awali ili anapoanza darasa la kwanza asipate shida kuanza kujifunza kusoma.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igoma, Juliana Madaha anasema mpango wa KKK umewasaidia kufuta ujinga kwa wanafunzi ambao walikuwa hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu.
Anasema shule ya Igoma ndio iliyozaa shule ya Samia ambapo baada kujengwa kwa madarasa mengine wakapunguza baadhi ya wanafunzi na kuhamia Samia.
Anasema tayari wameshapokea vifaa vya kufundishia na kujifunzia na miongozo ya mitaala kwa walimu waliopata mafunzo ya KKK.
Anasema kitendo cha kupatiwa vitabu vya kutosha kimesaidia kuwapo kwa uwiano ambapo kitabu kimoja husomea mwanafunzi mmoja.
Hata hivyo, anasikitishwa na baadhi ya wazazi kuwa na mwamko mdogo kuwaandisha watoto wao kuanzia shule za awali hivyo kuwafanya walimu wa darasa la kwanza kupata shida kuwaelewesha hadi kuelewa.
Akizungumzia Programu ya KKK, Ofisa Elimu Kata ya Kisigiri, Maryloyce Kileo anasema imefanikiwa kwa sababu walimu wamepatiwa mafunzo kabla ya kuanza kufundisha.
Anasema walimu wachache waliopata mafunzo walirudi shuleni na kuwafundisha wenzao, ndio maana hadi sasa programu hiyo inaendelea kuzaa matunda.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ofisa Elimu katika halmashauri hiyo, James Willium anasema mradi wa LANES umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani umewatoa watoto katika hatua za kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu hadi sasa wanaendelea kufanya vizuri.
WANAFUNZI WAONESHA UWEZO
Ili kujiridhisha na kile kinachozungumzwa kwamba KKK imezaa matunda, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Samia, aliwashangaza wageni waliofika shuleni hapo baada ya kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa kwa ufasaha na kujiamini.
Mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Kenedy Geofrey alikuwa akiulizwa maswali na mmoja wa maofisa elimu, James Willium ambapo aliyajibu bila kutetereka.
Pamoja na mambo mengine, Geofrey alisoma vema kitabu alichopewa hivyo kuthibitisha uwezo wake katika KKK.
Mtoto huyo alisoma kitabu cha Kingereza na Kiswahili.
Mara baada ya kumaliza kusoma na kuhesabu aliulizwa endapo akimuona Rais John Magufuli atamweleza nini?
Akajibu: “Niitamshukuru kwa kutuwezesha watoto kusoma bure.”
Veronica John wa Shule ya Awali Igoma, naye aliwashangaza watu mbalimbali baada ya kuonesha umahiri wake katika kusoma kwa kutambua herufi na hata kuandika.
Hii inadhihirisha kwamba elimu ya awali ni mwongozo wa mwanafunzi anayejiandaa kuingia darasa la kwanza.
MALENGO YA SERIKALI
Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha elimu inazidi kufanikiwa zaidi, hivyo ipo mbioni kukamilisha uanzishaji wa ofisi za takwimu katika halmashauri zote nchini ili kukusanya taarifa za elimu, kuzifanyia kazi na kuleta ufanisi.
Mratibu Msaidizi wa Programu ya Ujifunzaji na Ufundishaji wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Isack Kitururu anasema programu hiyo ilianza mwaka 2014 na kwamba inatarajiwa kumalizika Desemba 2018.
Anasema ipo chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden ambapo Dola za Marekani milioni 94.8 zimetengwa kuukamilisha.
Anasema tayari wizara imeshasambaza vitabu vya kujifunzia vya kutosha katika mikoa yote kwa ajili ya kujifunzia watoto kabla ya kuanza darasa la kwanza.
Anabainisha kuwa vitabu zaidi ya milioni 27.74 sawa na asilimia 62.72 vimeshachapwa na kusambazwa maeneo mbalimbali.
Hii inadhirisha kuwa kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa, kuna uwezekano wa wanafunzi wote nchini wakajua KKK tofauti na ilivyo sasa ambapo asilimia kubwa ya wanafunzi katika baadhi ya shule nchini hawajui kusoma.