NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imepanga kusikiliza utetezi wa kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara Yusuf Manji siku tatu mfululizo kuanzia Septemba 25 hadi 27 mwaka huu.
Manji jana alitakiwa kujitetea baada ya wakili wake, Hajra Mungula kudai walikuwa tayari kuendelea na utetezi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Hata hivyo Wakili Mkuu wa Serikali, Timony Vitalis alieleza mahakamani kwamba anataka kusafiri mchana , kesi imechelewa kuanza kusikilizwa hivyo hawezi kuendelea.
Hakimu Mkeha alimuuliza Manji kwanini alichelewa kwani kesi ilipaswa kuanza kusikilizwa saa tatu asubuhi ambapo Manji aliomba samahani lakini alidai alipitia hospitali na alikuwa akiwasiliana na wakili wake ambaye alimfahamisha kuwa hakimu yupo kwenye kikao.
Hakimu Mkeha alisema anaenda katika kikao mchana hivyo Wakili Mungula aliomba kesi ipangiwe siku tatu mfululizo kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa utetezi.
Manji anatarajia kuwaita mashahidi 15 na tayari shahidi mmoja ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alishatoa ushahidi.
Manji alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16, mwaka huu akidaiwa kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroine.