Na HILAL K SUED
KWA zaidi ya miongo miwili sasa nchi ya jirani yetu Kenya imekuwa mmoja wa wahanga wakuu wa kukosekana kwa hali ya utulivu nchini Somalia kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
Kenya inapakana na Somalia kwa upande wa Kaskazini-Mashariki. Ukaribu wetu na Kenya kihistoria, kisiasa na kijamii imetufanya pia kuwa katika mstari wa karibu na nchi hiyo katika suala zima la vurugu baina yake na Somalia.
Ni zaidi miaka miwili sasa tangu shambulio la kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo katika chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya ambapo zaidi ya watu 150, wengi wao wakiwa wanafunzi waliuawa na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabab cha Somalia katika tukio la kigaidi kubwa zaidi kuliko yote nchini humo tangu majeshi ya Kenya yaingie Kenya mwishoni mwa 2011 katika kile kilichoitwa ‘Operesheni Linda Nchi.’
Kusema kweli lilikuwa tukio kubwa kuliko yote katika eneo la Afrika Mashariki tangu yale ya ulipuaji ofisi za balozi za Marekani Nairobi na Dar es Salaam mwaka 1998.
‘Operesheni Linda Nchi’ ilibuniwa na kujitawala kwa Rais Mwai Kibaki kama jibu kwa matukio ya mara kwa mara ya ugaidi ya Al-Shabab dhidi ya watalii waliokuwa wakizuru Kenya kutoka nchi za Magharibi, matukio ambayo yalikuwa yakisababisha kuzorota kwa biashara ya utalii nchini humo ambayo ni tegemeo kubwa kwa uchumi wake.
Hivyo Kenya ilijikuta haina jinsi isipokuwa kufanya ilivyofanya kuokoa uchumi wake ingawa bila shaka ilijua athari zake. Na wengi waliona kwamba kitendo cha kupeleka majeshi nchini Somalia ni kama vile kujipalia mkaa kwani haikupita muda nchi hiyo, ilianza kuonja ulipizaji kisasi kupitia matukio ya kigaidi katika miji kadhaa, kubwa likiwa lile katika jengo la Westgate mjini Nairobi mwaka 2013 ambapo zaidi ya watu 70 waliuawa.
Hatua ya watawala wa Kenya kupeleka majeshi nchini Somalia kupitia eneo ambalo wanaishi watu wengi wa asili ya Kisomali halikukaa vyema kwa uendeshaji wa operesheni za kijeshi na katika kufanikisha kwake. Na ndiyo maana karibu miaka sita sasa hakuna mafanikio ya kuridhisha ya operesheni hiyo kwani AlShabab bado wanatamba katika maeneo ya pande zote mbili za mpakani na kufanya mashambulizi ya kigaidi ya mara kwa mara bila vikwazo vyovyote.
Lakini tukio la mauaji ya kigaidi dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa yalianza kuibua madai mapya kutoka kikundi hicho cha Alshabab, madai ambayo si mageni kwa wenye kuifahamu historia ya nchi ya Somalia. Mara tu baada ya shambulio hilo ambalo Al-Shabab walikiri kuhusika kupitia tamko lao, kiliweka madai ardhi ya Kenya.
Kama nilivyosema hili ni eneo la kaskazini linalopakana na Somalia na ambalo wanaishi watu wa asili ya Somalia (ethnic Somalis). Huko nyuma, tangu wakati wa ukoloni wa Uingereza, lilikuwa likijulikana kama North Frontier District (NFD) na ambalo baada tu ya Kenya kupata uhuru mwaka 1963, baadhi ya wakazi hao wakijulikana kama Mashifta na kusaidiwa na utawala wa Somalia, walianzisha mapambano na utawala mpya wa Rais Jomo Kenyatta kudai sehemu hiyo iingizwe Somalia.
Aidha inadaiwa kwamba kabla ya kutoa uhuru kwa Kenya, Uingereza iliendesha kura ya maoni katika eneo hilo la NFD iliyouliza iwapo wakazi wake wanataka kujiunga na Somalia au kubakia Kenya. Matokeo, ambayo hayakutangazwa, yalionyesha kwamba wengi walitaka kuwa chini ya Somalia.
Pengine kutokana na hili ndipo kulizuka vita vya Shifta (Shifta War), iliyodumu kati ya 1963 hadi 1967. Hili neno ‘shifta’ (yaani ‘haramia’ kwa lugha ya Kisomali) lilibuniwa na watawala wa Kenya na lilitumika zaidi kipropaganda.
Vikosi maalumu vya Kenya vya General Service Unit (GSU) vilifanya ukatili mkubwa dhidi ya hawa wapiganaji wa Kishifta. Wakazi wengi wa eneo hilo, hata wale ambao hawakuhusika walikamatwa na GSU na kuwekwa katika maeneo maalumu waliyoyaita maeneo ya ulinzi (protected areas) lakini hasa hasa yalikuwa ni makambi ya mateso tu (concentration camps) mithili ya zile kambi walizofungiwa wapiganaji wa Mau Mau chini ya wakoloni wa Uingereza miaka kumi nyuma.
Vita hivyo viliisha mwaka 1967 pale ambapo Muhammad Haji Ibrahim Egal, Waziri Mkuu wa Somalia wakati ule alipotia sahihi mkataba wa kuacha mapigano na utawala wa Kenya. Hata hivyo sehemu hiyo ya Kenya ilibakia na vidonda vikubwa na vitendo vya kiharamia vya hapa na pale viliendelea pamoja na madai mapya ya kutaka kujitenga kwa jimbo hilo. Lakini hatua za kibabe za serikali ya Kenya dhidi ya chokochoko hizo nazo pia zilionekana kufifia, lakini siyo kwisha kabisa.
Tofauti na huko nyuma kama nilivyotaja, madai haya ya sasa ya AlShabab hayana baraka ya serikali rasmi ya Somalia, ambayo sasa hivi ina changamoto nyingi mno kuliko kujiongezea hili jingine la madai ya ardhi ya nchi jirani. Isitoshe utawala wa Somalia unaiona Kenya kama swahiba na mdau mkuu katika mapambano yake dhidi ya Alshabab.
Lakini tangu uhuru wa Somalia (nchi ambayo ni muungano wa nchi mbili zilizokuwa zinatawaliwa na Uingereza na Italia) kulikuwapo kwa dhamira ya kuunda taifa kubwa la Somalia (Greater Somalia) ya kuyajumuisha pia maeneo mengine matatu ambayo yana watu wa asili ya Somalia, na ikibidi hata kwa kupigana. Maeneo haya ni hilo la NFD (Kenya), Ogaden (Ethiopia) na Afars and Issas (sasa Djibouti).
Wanadai kwamba ni katika kutimiza azma ya bendera ya Somalia ambayo ina nyota ya pembe tano. Pembe mbili tayari ndiyo Somalia zile mbili ambazo rasmi ziliungana na kupata uhuru mwaka 1960 na hizo tatu nyingine ni hayo maeneo yanayodaiwa. Mwaka 1977, chini ya utawala wa Jenerali Mohammed Siad Barre, Somalia iliivamia sehemu ya mashariki ya Ethiopia (jimbo la Ogaden) katika kutimiza dhamira ya kuunda Taifa Kubwa la Somalia.
Lakini baadhi ya wachunguzi wa mambo walisema Barre alifanya hivyo kwa uitikio wa msukumo wa Vita Baridi (Cold War) wakati huo ndiyo ilikuwa kigezo cha masuala mengi yaliyokuwa yakitokea katika nchi za Ulimwengu wa tatu pamoja na eneo hilo la Pembe ya Afrika.
Barre aliona kwamba anayo sapoti ya nchi za Magharibi kutokana na Ethiopia kuwa katika kambi ya nchi za mashariki, zile za Kikomunisti. Kusema kweli nchi hizi Somalia na Ethiopia), zilibadilishana kambi za kiitikadi baada ya kupinduliwa kwa Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia mwaka 1974. Haile Selassie alikuwa swahiba mkubwa wa nchi za magharibi katika eneo hilo na watawala wapya chini ya Kanali Mengistu Haile Mariam walibadili upepo na kukumbatia itikadi ya Kikomunisti.
Hata hivyo vita hiyo ya ogaden iliisha baada ya majeshi ya Somalia kurudishwa nyuma na hatimaye kuondoka kabisa katika ardhi ya Ethiopia.