25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU ALIVYOUMIA

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji, amesema Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alipigwa risasi wiki iliyopita mkoani Dodoma na watu wasiojulikana, amevunjika nyonga, miguu na mkono.

Alisema Lissu ambaye anatibiwa nchini Kenya, amevunjwa mguu wa kulia zaidi ya mara tano, mguu wa kushoto, nyonga na mkono wa kushoto.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Kinondoni, Dar es Salaam jana kuhusu hali ya Lissu, Dk. Mashinji alisema anaendelea vizuri ingawa juzi hali ilibadilika ghafla.

“Tuliambiwa alipigwa risasi tano mwilini mwake, lakini kwa jinsi mwili ulivyobomolewa, yawezekana zilizidi. Risasi ni za kivita halafu ziupate mwili wa mtu, tunategemea nini kitaendelea?

“Jana (juzi) saa 4 asubuhi, alianza kupata matatizo ya kifua, hali ilibadilika ikabidi madaktari wamwekee mashine ya kupumulia. mchana ilitengemaa wakaitoa.

“Madaktari walianza kumtibu sehemu za ndani ambazo zingeweza kuhatarisha maisha yake na wamemaliza. Awamu iliyofuata walianza kuunganisha mifupa kuanzia mkononi.

“Alifanyiwa upasuaji mara tatu, tumelazimika kusitisha operesheni ili aweze kupumzika. Wamemuumiza  mno na tulitegemea atatibiwa kwa muda mfupi na kurudi nyumbani, lakini kwa namna alivyoumia, itachukua muda mrefu… naomba tujiandae kama chama,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema pia licha ya kuongezewa chupa za damu mjini Dodoma kabla ya kupelekwa Nairobi, bado anaendelea kuongezewa.

Dk. Mashinji, alisema kitendo alichofanyiwa Lissu ni cha kinyama na kwamba hawaamini kama waliohusika wanastahili kuwa sehemu ya jamii.

“Bado najisikia uzito kuelezea jamii ya Watanzania hali ya Lissu inavyoendelea. Ni majonzi makubwa na kama kuna mtu katika taifa hili alifanya hicho kitendo, anatakiwa ajitafakari sana… inatia hasira sana,” alisema.

Dk. Masinji alisema kutokana na tatizo lililompata, hali yake haitakuwa sawa kama alivyokuwa kabla ya kushambuliwa kwa risasi.

 

FEDHA ZILIZOCHANGWA

Kuhusu fedha zilizochangwa, alisema hadi sasa zimechangwa Sh milioni 21.4 kupitia akaunti ya chama na nyingine ambazo zilitumwa kupitia simu za mkononi.

“Gharama za matibabu ni kubwa, tutatumia resources (rasilimali) zote za chama kuhakikisha Lissu anapona, anakuwa na afya njema,” alisema.

 

VILIO VYATAWALA

Wakati Dk. Mashinji akielezea maendeleo ya hali ya Lissu, baadhi ya viongozi na wanachama waliokuwapo katika mkutano huo, walishindwa kujizuia na kuanza kulia.

Miongoni mwa walioangukia kilio ni kada wa chama hicho, Mariam Sepetu ambye alishindwa kujizuia.

 

PROFESA ABDALLAH SAFARI

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Aballah Safari, alisema hawana imani na Jeshi la Polisi wala Serikali, hivyo wametaka kuwapo wapelelezi huru kutoka nje kuchunguza tukio hilo.

“Hatuna imani na Jeshi la Polisi na hatuwezi kuliachia liwatafute watu waliotaka kumuua Lissu, Serikali ikubali sasa wapelelezi wa nje waje kuwasaidia. Kama itakataa kuwaleta, basi wao watakuwa wanajua waliotaka kumdhuru.

“Tunaiomba jumuiya ya kimataifa kusaidia ili haki si tu kwamba itendeke, bali inatakiwa ionekane imetendeka,” alisema Profesa Safari.

Kwa mujibu wa Profesa Safari, kifungu namba 122 cha Sheria ya Ushahidi, kinazungumzia dhana zinazoruhusiwa na mahakama ama mtu kama kuna matukio yametokea, kwamba huwa kuna dhana chanya na hasi.

“Dhana hasi hapa ni kwamba polisi na Serikali inahusika na tukio la kutaka kumuua Lissu. Kifungu cha 10 cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) kinaeleza namna polisi inavyotakiwa kufanya kazi zao.

“Kuna suala la kutoa taarifa, asilimia 90 ya watu huwa hawaendi. Lissu alitoa taarifa, lakini polisi hawakujali,” alisema.

 

BENSON KIGAILA

Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Benson Kigaila, alisema Kamati Kuu ya chama hicho ilikutana wiki iliyopita na kujadili mtiririko wa matukio mbalimbali yaliyotokea tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.

“Hakuna aliye salama, tusidanganyane. Lissu alipigwa risasi kikatili akiwa ameegesha gari nyumbani kwake, mahali ambako pia wanaishi wabunge, mawaziri na naibu Spika. Na eneo lile lina geti na walinzi wenye silaha, halafu wanataka kutuambia hawawajui?” alihoji Kigaila.

Alisema kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kulinda raia na mali zao, lakini havina mamlaka ya kuwazuia Watanzania wasijadili masilahi yao.

“Viongozi wawe tayari kusikiliza wananchi na majeshi yalinde usalama wa raia,” alisema Kigaila.

 

Mwisho.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles