NA JESSCA NANGAWE
WAKATI kipa wa Simba, Said Mohammed Nduda akitarajiwa kuondoka wiki ijayo kuelekea India kwa matibabu, beki wa timu hiyo, Shomary Kapombe, atarejea uwanjani kuanza mazoezi mepesi.
Kapombe na Nduda ameendelea kukosa mechi za awali za Ligi Luu kutokana na kuwa majeruhi tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Simba, Haji Manara, alisema Kapombe anatarajia kuanza mazoezi wiki ijayo, baada ya kumaliza matibabu yake kutokana na majeraha aliyopata wakati akitumikia timu ya Taifa (Taifa Stars).
“Kapombe anaendelea vyema na matibabu na kwa mujibu wa daktari atakuwa fiti kuanzia Jumatatu, anaweza kuanza mazoezi mepesi ili kurudi kwenye kiwango chake kama kawaida,” alisema Manara.
Alisema kwa upande wa Nduda, ataelekea nchini India mara baada ya taratibu za safari na hospitali atakapofikia kukamilika.
Kipa huyo bora wa michuano ya COSAFA mwaka huu nchini Afrika Kusini alisajiliwa na Simba akitokea Mtibwa, aliumia katika kambi ya Zanzibar wakati wakijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wao, Yanga.
Wachezaji hao tangu wasajiliwe na klabu hiyo hawajawahi kuitumikia timu hiyo katika michezo yake ya ligi, kutokana na kuwa majeruhi.