33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI WALIOTAJWA RIPOTI ZA MADINI WATAKIWA KUJISALIMISHA POLISI

PATRICIA KIMELEMETA na JULIETH PETER – DAR ES SALAAM/MANYARA

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amewataka watuhumiwa waliotajwa katika Ripoti za Kamati za Bunge za kuchunguza madini ya tanzanite na almasi kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boazi, ili wahojiwe.

Uamuzi huo umekuja baada ya juzi Rais Dk. John Magufuli kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwaita na kuwahoji  watuhumiwa wote waliotajwa katika ripoti hiyo, ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Katika ripoti hiyo, ambayo Magufuli alikabidhiwa Ikulu, Dar es Salaam juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baadhi ya viongozi waliotajwa ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani na Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Frederick Werema.

Wengine ni Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Manyara ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alisema hakuna haja ya kuwataja majina watuhumiwa hao kwa sababu tayari walishatajwa katika ripoti hiyo na akawataka kutumia busara na hekima kufika wenyewe katika ofisi hizo zilizopo Dar es Salaam katika makao makuu ya jeshi hilo ili waweze kuhojiwa.

“Kuna baadhi yao wameanza kupiga simu ya kutaka kujua utaratibu wa kufika ofisi zetu, tumewaambia waje kwa DCI ili waweze kuhojiwa, hatuoni sababu ya kutajana majina wakati wanajijua,” alisema.

Alisema ikiwa watakaidi taarifa hizo, watakamatwa kwa nguvu na kufikishwa katika ofisi hizo kwa ajili ya kusubiri hatua nyingine za kisheria.

“Hakuna haja ya kukamata wakati wanajua kuwa wamo kwenye ripoti, tunawaomba wafike ofisini ili tuweze kuwahoji na si kusubiri kukamatwa,” alisema.

Pia alisema jeshi hilo linafuata maelekezo waliyopewa na Magufuli wakati alipokabidhiwa ripoti hiyo na hadi sasa kuna baadhi ya watu wametii agizo hilo na kufika katika ofisi za jeshi hilo ili wahojiwe.

Pia alisema tayari wameshawakamata baadhi ya watu waliotajwa wanaoishi mkoani Arusha na mahojiano bado yanaendelea.

“Kuna baadhi ya watu waliotajwa kwenye ripoti hiyo ambao tayari tumeshawakamata na mahojiano yanaendelea, hivyo basi waliobaki wanapaswa kufuata taratibu za kisheria,” alisema.

Katika hatua nyingine, Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One iliyopo Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Hussein Gonga na Faisal Juma, wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Masawe, alithibitisha kukamatwa kwa wamiliki hao, huku akisisitiza kwamba jeshi hilo linaendelea kuwasaka wamiliki wengine.

“Ni mapema kutoa taarifa ambazo bado hazijakamilika, zikikamilika nitawapa kila kitu. Hata kama tumemkamata mmoja, hadi sasa lengo letu ni kuwakamata wamiliki wengine zaidi,” alisema Massawe na kuongeza:

“Tumewakamata kwa ajili ya mahojiano, suala hili ni pana, siwezi kuingia kwa undani zaidi hadi tutakapokamilisha.”

Kampuni ya Tanzanite One iliyokuwa ikimilikiwa awali na mwekezaji kutoka Afrika Kusini, iliuzwa hisa zake na kununuliwa na wazawa Gonga, Juma na raia mwingine wa kigeni kutoka India, anayejulikana kwa jina moja la Riziwan.

Kupitia kampuni yao ya Sky Associate, wazawa hao walianza kuendesha mgodi huo kwa ubia na Shirika la Madini Tanzania (Stamico), lakini tangu wamenunua mgodi huo kumekuwapo na malalamiko, ikiwamo migogoro dhidi yao na wachimbaji wadogo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles