ABDUCADO EMMANUEL, DAR NA MICHAEL MAURUS, MTWARA
SAKATA la winga wa timu ya Yanga, Simon Msuva kwenda kufanya majaribio Afrika Kusini kwenye timu ya Bidvest Wits bila ruhusa ya uongozi wake, limechukua sura mpya baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom kuishtaki timu hiyo kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Msuva aliyerejea nchini juzi baada ya kumaliza majaribio hayo na kudaiwa kufanya vizuri, alitorokea nchini humo Jumatatu iliyopita usiku bila kuafikiana na uongozi wa Yanga.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, aliliambia MTANZANIA jana kuwa kutokana na Bidvest kuvunja sheria za usajili za Fifa, tayari wameshaishtaki huko tokea Alhamisi iliyopita ili wakubwa hao wa soka waiadhibu kwa ukiukaji huo.
“Tokea tuwatumie barua hiyo Fifa bado hawajatupa majibu yoyote, ila kwa mujibu wa taratibu za shirikisho hilo, linaweza kuamua suala hilo hata baada ya miezi miwili ijayo pale watu mnapokuwa mmesahau,” alisema.
Alisema mpaka sasa hakuna mawasiliano yoyote waliyopata kutoka Bidvest, huku akieleza kuwa watalitolea ufafanuzi suala hilo kwa kina kesho.
Msuva aliyebakiza mkataba wa mwaka mmoja ni kinara wa mabao wa timu hiyo msimu huu kufuatia kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa mabao 17.
Fifa inakataza timu yoyote kuanza mazungumzo na mchezaji wa timu nyingine aliye na mkataba wa zaidi ya miezi sita na timu yake bila ruhusa ya uongozi wa timu husika.
Akizungumzia mipango ya timu hiyo baada ya ligi kumalizika, Tiboroha alisema timu nzima ipo mapumzikoni hivi sasa hadi Mei 30 mwaka huu itakapokusanyika tena, huku Kocha Mkuu, Hans van Pluijm na wachezaji wote wa nje ya nchi wakitarajia kuondoka nchini kesho.
Si mara ya kwanza kwa Yanga kupeleka malalamiko Fifa, mwaka jana iliwahi kufanya hivyo kwa kuishtaki Wadi Degla ya Misri iliyowahi kufanya mazungumzo na mshambuliaji wao wa zamani, Emmanuel Okwi bila ridhaa yao, ambapo Wanajangwani hao walihitaji fidia ya Dola za Kimarekani milioni moja.
Lakini mpaka sasa Fifa haijatoa majibu na Okwi tayari amehamia Simba toka kuanza kwa msimu uliopita.
Pluijm ashikilia usajili
Wakati huo huo, taarifa kutoka Mtwara ilipocheza timu hiyo dhidi ya Ndanda, zinaeleza kuwa Pluijm ndiye ameshikilia usajili wa timu hiyo kwa msimu ujao kuhusu wale wa kubaki na kutemwa pamoja na usajili wa wachezaji wapya.
Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu baada ya kujikusanyia pointi 55, huku ikikata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Pamoja na kutwaa ubingwa huo mikononi mwa Azam, Yanga imepanga kukisuka upya kikosi chao ili iweze kuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa.
Akizungumza na gazeti hili mjini hapa juzi, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema: “Tunashukuru ligi imemalizika na tumetwaa ubingwa, juu ya wachezaji watakaobaki au kuachwa, hilo litategemea na ripoti ya mwalimu atakayoitoa kwa uongozi, hivyo tusubiri kidogo muda si mrefu, mambo yatakuwa hadharani.”
Licha ya kutwaa ubingwa, Yanga mwaka huu imeishia raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa jumla ya mabao 2-1, awali ilizitoa BDF XI ya Botswana (3-2) na FC Platinum ya Zimbabwe (5-2).