25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TAIFA STARS IONYESHE MWELEKEO AFCON 2019

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imeifunga Botswana mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, uliochezwa juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mchezo huo upo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Katika viwango vya ubora vitolewavyo na Fifa, vilivyotolewa Julai mwaka huu, Tanzania inashika nafasi ya 120 wakati Botswana ikishika nafasi ya 140.

Stars kwa sasa inaonekana kama inasukwa upya ikiwa chini ya Kocha Mkuu Salum Mayanga, ambaye alichukua mikoba ya kukinoa kikosi hicho Machi mwaka huu kutoka kwa Charles Boniface Mkwassa.

Hadi mechi ya juzi, Stars imefikisha mechi 12 chini ya Mayanga, ikishinda sita, sare tano na kupoteza moja.

Ushindi huo wa Stars unaanza kuleta faraja kwa Watanzania ambao wamepoteza imani na timu yao hiyo kutokana na kufanya vibaya katika mechi za kimataifa, hasa za kusaka fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na Kombe la Dunia.

Sisi MTANZANIA tunalipongeza benchi la ufundi la Stars chini ya Mayanga, lakini pia kulipa angalizo la kuindaa timu hiyo ili ionyeshe mwelekeo wa kufuzu AFCON ya 2019 itakayofanyika nchini Cameroon.

Wachezaji walio katika timu hiyo wakiongozwa na nahodha wao Mbwana Samatta, anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji, sambamba na wachezaji wengine wanaocheza soka nje ya Tanzania na wale wanaocheza ligi ya Tanzania, wanaonekana kufahamu majukumu yao vema na dhamira ya baadae.

Stars ambayo imeshiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza nay a mwisho mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria, haijawahi kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia tangu zilipoanzishwa mwaka 1930.

Mayanga anaweza kuvunja rekodi ya mwaka 1980, iwapo ataivusha Stars kwa kuiwezesha kushiriki AFCON 2019 nchini Cameroon.

Akifanikiwa, jina lake litabaki katika rekodi na kusomwa kama kumbukumbu na vizazi  vijavyo kwa kuwa atakuwa ameteitendea haki taaluma na Tanzania kwa ujumla.

Mwelekeo wa Stars ya Mayanga unaridhisha hadi sasa na iwapo atapata mechi nyingi za kimataifa dhidi ya nchi zilizo juu katika viwango vya ubora vya Fifa, bila shaka itafikia mafanikio ya kufuzu AFCON 2019.

Sisi MTANZANIA tunamuunga mkono Mayanga katika safari yake aliyoanza nayo kueleka kusaka nafasi ya kufuzu AFCON 2019 nchini Cameroon.

Tumeona kikosi cha Stars kinavyoimarika kadiri muda unavyokwenda, lakini kinahitaji mechi nyingi za kimataifa ili kiweze kuwa na ubora zaidi wa kushinda na kufuzu.

Ni wakati wa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, chini ya Waziri Dk. Harisson Mwakyembe, kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadhamini wakuu wa timu hiyo, ili Stars iwekewe mikakati ya kufuzu AFCON.

Iwapo mikakati madhubuti itaandaliwa, ni imani yetu kuwa Stars itafikia mafanikio ya juu zaidi na kuwa tishio katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika na Dunia kwa ujumla kutokana na kucheza soka la kuvutia litakalotishia nchi nyingine zilizoendelea katika mchezo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles