Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Kairuki imewasilisha utetezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikipinga madai ya kumsababishia madhara ya afya, Khairat Omary.
Katika utetezi huo uliowasilishwa mahakamani hapo mwishoni mwa wiki, hospitali hiyo inadai haihusiki na madhara wala hasara aliyoipata mdai katika kesi ya madai namba 184 ya mwaka huu.
Hospitali hiyo imedai hayo kupitia hati yake ya utetezi ikiwa imeambatanishwa na vielelezo mbalimbali ilivyoviwasilisha mahakamani kupitia wakili wake, Mohammed Tibanyendera wa Kampuni ya Uwakili ya Star.
Inadaiwa hatua ya mdai kuhudumiwa katika hospitali zisizo za utaalamu baada ya kujifungua na kutorudi kwenye hospitali hiyo kwenda kutibiwa, ndiyo chanzo cha madhara yaliyomkuta.
Katika utetezi wake hospitali hiyo imekiri Khairat alikuwa mteja wake na alikuwa akihudhuria kwenye hospitali hiyo iliyoko Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti wakati wa ujauzito wake na baada ya kufanyiwa upasuaji Desemba 15, mwaka jana.
Hata hivyo, hospitali hiyo imekataa kulipa gharama zilizoombwa na mdai kwa kuwa madai hayo hayana msingi na hayatekelezeki na imemtaka ayathibitishe.
“Wakati mlalamikaji akihudhuria hospitalini, gharama zote zilikuwa zikibebwa na kulipwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia namba ya uanachama 202601295913.
“Mlalamikaji alikuwa na matatizo katika ujauzito kiasi cha kwamba asingeweza kujifungua kwa njia ya kawaida bali kwa upasuaji.
“Mlalamikaji aliridhia na kutia saini kiapo cha kukubali kufanyiwa upasuaji Desemba 15, mwaka jana,” ilidai sehemu ya hati ya utetezi.
Mdaiwa anadai Desemba 21, mwaka jana, mdai alionwa na daktari kwa ajili ya kujua maendeleo ya afya yake na alikuwa akiendelea vizuri licha ya kuwa na maumivu sehemu za mshono na wala hakuwa na usaha kwenye sehemu ya jeraha.
Hati hiyo ya utetezi inadai siku hiyo hiyo mdai alifanyiwa uchunguzi wa afya na kuonekana anaendelea vizuri na kizazi chake kilikuwa vizuri katika wiki ya 16.
“Siku chache kabla ya mdai kujifungua, Desemba 5, mwaka jana, alikutwa na UTI ambako hospitali ilimpatia matibabu.
“Alikuwa na historia ya kupata maumivu ya tumbo na mgongo ambayo hayahusiani na upasuaji aliofanyiwa Desemba 15, mwaka jana.
“Hospitali inakataa madai ya mdai kwamba ilikiuka wajibu wake wa utoaji huduma ya afya kuhakikisha hatua za awali za uchunguzi, licha ya mdai kueleza wasiwasi wake juu ya afya yake,”ilidai hati ya utetezi.
Hospitali hiyo inakataa madai kwamba mdai alifika hospitali hapo baada ya kujifungua na kutoa malalamiko yake kuwa alikuwa anatapika na kusikia kichefuchefu.
“Hakuna vifaa vyovyote vya kujifungulia vilivyoachwa kwenye mfuko wake wa uzazi kwa sababu Desemba 21, mwaka jana, alifanyiwa kipimo cha ultrasound kwenye hospitali hiyo.
“Madhara kwa mdai yalipatikana baada ya kuhudhuria hospitali zisizo za utaalamu kwa matakwa yake bila kuishirikisha hospitali hiyo,” ilidai hati hiyo ya madai na kuongeza kwamba madai kuwa hawezi kupata mtoto tena hayaihusu hospitali hiyo na sababu atakuwa anazijua mwenyewe mdai.
Kwa sababu hiyo, hospitali hiyo inasisitiza kuwa hakuna dai la sheria lililoko mahakamani.
Hospitali inapinga madai ya mdai kuomba mahakama imwamuru amlipe Sh milioni 155 hivyo imeiomba mahakama kuiondoa kesi hiyo kwa gharama.
Khairat kupitia wakili wake, Jonas Nkya, alifungua kesi hiyo ya madai mahakamani hapo, dhidi ya Hospitali ya Kairuki, akiomba iamriwe kumlipa Sh milioni 155.
Anadai kwamba baada ya hospitali hiyo kumfanyia upasuaji Desemba 15, mwaka jana, ilimuacha na vifaa vya kujifungua kwenye mfuko wa uzazi jambo ambalo lilifanya kizazi kiharibike na kutolewa.
Kesi hiyo ya madai iliyofunguliwa na Khairat dhidi ya hospitali hiyo, iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Ilitajwa kwa mara ya kwanza Agosti 31, mwaka huu na iliahirishwa hadi Septemba 18, mwaka huu.