29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAHABARI MUHINGO RWEYEMAMU KUZIKWA KESHO

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MWANAHABARI mkongwe na mkuu wa wilaya mstaafu, Muhingo Rweyemamu ambaye alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Aga Khan   Dar es Salaam, atazikwa katika makaburi ya Kinondoni kesho.

Muhingo alikutwa na mauti wakati akitibiwa katika hospitali hiyo, akisumbuliwa na ugonjwa wa Myelofibrosis ambao hudhoofisha uwezo wa kinga za mwili kutengeneza damu.

Akizungumza na MTANZANIA, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda ambaye pia alikuwa rafiki wa marehemu, alisema baada ya kikao cha mashauriano, imekubaliwa kwamba  Muhingoi atazikwa kesho.

“Shughuli za mazishi zitatanguliwa na ibada ya kumuaga ambayo itafanyika katika Kanisa la KKKT Mbezi (Kibanda cha Mkaa).

“Mwili wa marehemu Muhingo unatarajiwa kufikishwa nyumbani kwake Mbezi Luis Jumatatu ambako utalala hadi  Jumanne.

“Ratiba ya shughuli nzima na taratibu kamili za mazishi zinatarajiwa kutolewa kesho (leo) Jumatatu,”alisema Kibanda.

Akizungumza juzi na gazeti hili, Msemaji wa familia ambaye pia ni kaka wa marehemu, Elisa Muhingo, alisema kwa   takribani miaka 11, Muhingo alikuwa anaumwa na kuwekewa damu mara kwa mara na kwamba mwaka jana alizidiwa.

Enzi za uhai wake, Muhingo alitambulika vema kama mwalimu mbobezi na kiongozi mahiri katika masuala ya habari kwa waandishi wengi ambao wanaendelea kuitumikia tasnia hiyo. Pia ni mmoja wa waanzilishi wa gazeti la Mwananchi.

Umahiri wake ndani ya tasnia ya habari ulijitanua na kufahamika vema kuanzia mwaka 1993 alipoanza kuripoti kwenye magazeti ya Mwananchi na The Express.

Mazingira ya kubobea zaidi katika uandishi yalimpandisha hadhi mwaka 1995 na kuwa mwandishi mwandamizi, Mhariri wa Makala, Mhariri na Mkuu wa Kitengo cha Picha katika Gazeti la Mtanzania.

Ndani ya utumishi wake katika ngazi ya uhariri, Muhingo, alitumikia magazeti mbalimbali   nchini na baadaye kuwa  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.

Mbali na ubobezi wake katika tasnia hiyo, pia Muhingo amepata kutumikia nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Makete na Morogoro Mjini.

 

WASIFU

Mwaka 2004 Muhingo alihitimu masomo ya Shahada ya Kwanza ya Uandishi wa Habari (BAJ) katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa.

Mwaka 1993 alihitimu Stashahada ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha TSJ.

Mwaka 1989 alihitimu Stashahada ya Elimu katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dar es Salaam.

Mwaka 1983 alihitimu Astashahada ya Elimu katika Chuo cha Ualimu cha Tukuyu na mwaka 1977 alihitimu Elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Nyakato.

UZOEFU KAZINI

Mwaka 1984-1985 alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Igwata, Geita.

Mwaka 1985-1987 alikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makongo, Dar es Salaam.

Mwaka 1989 alikuwa Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Mwaka 1989-1992 alikuwa Katibu Uenezi Taifa wa Chama cha Wanataaluma ya Uenezi.

Mwaka 1993-1995 alikuwa mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na The Express.

Mwaka 1995-1998 alikuwa Mwandishi Mwandamizi , Mhariri wa Makala, Mhariri na Mkuu wa Kitengo cha Picha katika Gazeti la Mtanzania.

Mwaka 1999 alikuwa Mhariri Mkuu wa Jarida la Wiki Hii.

Mwaka 1999-2001, alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi.

Mwaka 2003, alikuwa Mwakilishi wa Jarida la habari za mazingira la ENS la Marekani.

Mwaka 2004-2005, alikuwa Mhariri Mshiriki akihusika na mambo ya siasa katika Gazeti la Citizen.

Mwaka 2006-2008 alikuwa Mhariri wa Gazeti la Rai.

Mwaka 2008-2010, alikuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles