NA SOSTHENES NYONI
ACHANA na Mbwana Samatta wa KR Genk ya Ubelgiji, Elias Maguli wa Dhofar SC ya Oman, Farid Musa anayekipiga Teneriffe ya Hispania na Abdi Banda, anayeichezea Baroka FC, Watanzania leo wana shauku ya kumshuhudia kiungo Simon Msuva, anayetarajia kuichezea timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa mara ya kwanza itakapoumana na Botswana, tangu alipojiunga na klabu ya Difaa Al Jadid ya nchini Morocco.
Stars na Botswana zitashuka dimbani kukabiliana katika pambano la kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), litakalopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Msuva alijiunga na Al Jadid wakati wa dirisha la usajili la msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea kwa mabingwa wa Tanzania, Yanga aliyodumu nayo kwa misimu mitano baada ya kujiunga nao mwaka 2012.
Akiwa na Yanga alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne, huku mara tatu ikiwa mfululizo.
Makali yake hayakuishia Yanga pekee, pia kwa muda mrefu amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Taifa Stars, ambapo Julai mwaka huu alikisaidia kushika nafasi ya tatu kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa) iliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Moto aliouwasha katika Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa ameuhamishia Morocco kwani licha ya kuwa hana muda mrefu lakini tayari ameonyesha makeke baada ya kuonyesha kiwango maridadi na kufunga mabao kadhaa akiwa na kikosi cha Al Jadid katika mechi za kirafiki kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya nchini humo.
Msuva pia hivi karibuni aliisaidia Al Jadid kufuzu raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Ligi Morocco, maarufu kama Throne Cup baada ya kufunga bao moja kati ya matatu yaliyowapa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya CR Khemis Zemamra.
Ubora wake aliouonyesha kwa muda mfupi nje ya mipaka ya Tanzania, ndio ambao mashabiki wa soka wa hapa nchini wanataka kuona akiendeleza leo kama atafanikiwa kupangwa katika kikosi cha Taifa Stars.
Imani yao ni kwamba, muunganiko kati yake na washambuliaji; Mbwana Samatta na Elias Maguli, katika eneo la ushambuliaji utaisaidia Taifa Stars kupata matokeo chanya leo itakapoumana na Botswana.
Zaidi hapo, kama ataendeleza ubora wake katika kikosi cha Taifa Stars, ni wazi itazidi kumfungulia njia ya kuyasaka mafanikio zaidi na kutimiza ndoto zake za kucheza soka barani Ulaya na kuungana na Samatta pamoja na Mussa.
Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, alisema kikosi chake kipo timamu kimwili na kiakili tayari kwa kuivaa Botswana na kuibuka na ushindi.
“Mimi kama kocha nimekamilisha wajibu wangu wa kuiandaa timu kimbinu na kiufundi, kilichobaki ni wachezaji nao kutimiza wajibu wao.
“Nawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kuja kuiunga mkono timu yao, naamini kwa kufanya hivyo wataongeza morali ya wachezaji na hatimaye tuweze kupata matokeo mazuri,” alisema Mayanga.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Stars kuumana na Botswana ndani ya mwaka huu pekee, ambapo Machi 25 timu hizo zilikutana katika mchezo wa kirafiki ukipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Samatta.
Katika viwango vya ubora wa soka duniani vilivyotolewa kwa mara ya mwisho na Fifa, Stars ipo nafasi ya 120, wakati Botswana inakamata nafasi ya 126.