NA TWALAD SALUM, MISUNGWI
WANAFUNZI 712 waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu Misungwi, mkoani Mwanza, bado hawajaanza masomo yao katika shule 23 za sekondari.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Misungwi, Tabu Makanga.
Alisema wanafunzi waliofaulu kwenda sekondari ni 3,884 na kati ya hao, 700 hawajaripoti katika shule walizopangiwa, huku 12 wakiwa wamehamishiwa shule nyingine kwa taratibu za kisheria.
Alisema wavulana waliofaulu na kutakiwa kwenda kidato cha kwanza ni 1,932 na kati ya hao, 290 hawajaripoti, huku wasichana waliochaguliwa ni 1,940, lakini ambao hawajafika shuleni ni 422.
Alizieleza sababu za wanafunzi hao kutofika shuleni ni uelewa mdogo wa baadhi ya wazazi kuhusu elimu, kuolewa na kuongeza kuwa watendaji wa vijiji na kata wanachangia kutowajibika ipasavyo, huku baadhi yao wakipokea rushwa kutoka kwa wazazi hao.
“Mzazi anapotozwa faini na viongozi wa kata au kijiji ya kutompeleka mtoto shule, wanaona wamepewa adhabu ya mwisho ya kutompeleka mtoto shule na kubaki nyumbani, sababu nyingine kwa watendaji ni kupokea rushwa, hili ni tatizo kubwa katika wilaya hii,” alisema Tabu.