NEW YORK, MAREKANI
BINGWA namba moja wa zamani wa mchezo wa tenisi kwa upande wa wanawake, Angelique Kerber, ametolewa kwenye mashindano ya US Open baada ya kuchezea kichapo kutoka kwa mpinzani wake, Naomi Osaka mwenye umri wa miaka 19.
Bingwa huyo mtetezi wa mashindano hayo ya wazi, ametupwa nje kwa seti 6-3, 6-1, katika raundi ya kwanza. Angelique ambaye aliwahi kuwa namba moja Septemba mwaka jana huku akiwa na umri wa miaka 28, ameshindwa kutetea taji lake.
Alikutana na upinzani wa hali ya juu kutoka kwa Naomi ambaye anashika nafasi ya 798 kwa ubora wa viwango vya tenisi duniani, wakati huo Angelique akishika nafasi ya sita, lakini baada ya kupoteza mchezo huo wa juzi atakuwa nje ya 10 bora.
Kupoteza mchezo kwa nyota huyo ni mwendelezo mbaya baada ya kuondolewa kwenye raundi ya kwanza katika michuano ya wazi ya Ufaransa mapema mwaka huu. Kwa upande wa Naomi ni historia kubwa kushinda mbele ya bingwa huyo.
“Ushindi huu una maana kubwa sana kwa upande wangu, haikuwa kazi rahisi kupambana na mpinzani huyo, lakini ninashukuru nimeweza kushinda na kusonga mbele.
“Ninaamini hali hii ya ushindi itaendelea hadi hatua ya mwisho kwa kuwa nimefanya maandalizi mazuri na lengo langu ni kuja kushinda na kuweka historia mpya katika maisha yangu ya mchezo huu,” alisema Naomi.
Kwa upande wa Angelique, amedai kusikitishwa na kiwango alichokionesha kwenye mchezo huo. “Sikutarajia kucheza chini ya kiwango, nilijiandaa kwa ajili ya kufanya vizuri, lakini nimejikuta katika wakati mgumu mbele ya mashabiki zangu.
“Mwaka huu umekuwa mgumu sana kwangu, sikuweza kufanya vizuri kwenye michuano ya wazi ya Ufaransa na nimekuja kufanya hivyo hapa kwenye US Open, ila nampongeza mpinzani kwa ushindani wake,” alisema Angelique