26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

AVEVA, KABURU ‘WATUA’ KWA MTAALAMU WA MAANDISHI

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

JAMHURI imedai kuwa bado inaendelea kuchunguza nyaraka mbalimbali zilizokusanywa na kupelekwa kwa mtaalamu wa maandishi katika kesi inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu.

Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.

Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili Wilson, baada ya kudai hayo aliomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kesi iliahirishwa hadi Septemba 8, 2017 na Hakimu Nongwa aliamuru upande wa mashtaka kuharakisha ripoti hiyo ili kesi iendelee.

Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha Dola za Marekani 300,000.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15, 2016 katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakati akijua ni kosa.

Katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, 2016 Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za Marekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15, 2016 katika Benki ya Barclays Mikocheni alijipatia Dola za Marekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika Benki ya Barclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia Dola za Marekani  300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles