Na PATRICIA KIMELEMETA -DAR ES SALAAM
AJIRA ni janga la kitaifa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya maelfu ya vijana jana kujitokeza katika usaili wa kuomba nafasi 400 za kazi zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Usaili huo ulifanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya vijana 56,000 walijitokeza kuwania nafasi hizo za ajira.
Usaili huo uliendeshwa na Sekretarieti ya Ajira kwa kuwapa mtihani maalumu wa kuandika, huku maelefu ya vijana hao wakionekana kusongamana kutokana na wingi wao.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema TRA ilitangaza nafasi za kazi 400, lakini idadi ya watu waliojitokeza ni kubwa nafasi zenyewe.
Alisema hali hiyo inaonyesha wazi kuwa, kuna mwamko wa watu kufanya usaili wa ajira kuliko ilivyokua awali, ambapo baadhi ya watendaji wasio waadilifu wamekuwa wakitumia nafasi hizo kwa ajili ya kuwaweka ndugu au jamaa zao.
“TRA ilitangaza nafasi 400, lakini idadi ya watu waliojitokeza ni kubwa kuliko tulivyokusudia, jambo ambalo linaonyesha kuna mwamko wa watu kujitokeza kufanya usaili wa ajira, tofauti na miaka iliyopita,” alisema Kayombo.
Alisema kwa sasa Serikali imeipa Sekretarieti ya Ajira iliyopo chini ya Wizara ya Utumishi jukumu la kusimamia ajira zinazotangazwa serikalini, tofauti na zamani ambapo taasisi na idara za serikali zilikuwa zinaajiri kivyake.
Kayombo alisema watakaobahatika kupata ajira hizo ni wale watakaofaulu mitihani iliyotolewa na Sekretarieti ya Ajira kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
“Lengo letu ni kuhakikisha watakaoajiriwa ni wale wenye sifa, hali ambayo itasaidia waombaji kupata haki sawa katika nafasi za ajira zilizopo, kuondoa mazingira ya upendeleo,”alisema.
Hata hivyo, baadhi ya vijana waliojitokeza kufanya mtihani huo wamesema lengo lao ni kujaribu bahati kama wanaweza kupata nafasi hizo au laa.
“Tumekuja hapa kwa ajili ya kufanya usaili, hatujui kama tutapata au laa, kwa sababu idadi ya watu waliojitokeza ni wengi, lakini binafsi siwezi kukata tamaa kwa sababu naamini naweza kufanikiwa,” alisema Joseph David.
Naye Rosemary Herman, alisema amejitokeza uwanjani hapo kwa ajili ya kufanya usaili huo akiamini kuwa anazo sifa zinazohitajika.
“Unajua ajira sasa ni ngumu, idadi kubwa ya vijana tupo nyumbani baada ya kumaliza masomo, hivyo tuliposikia nafasi zimetangazwa, kila mmoja anahangaika kuomba ili aweze kujaribu bahati yake,” alisema.
Wiki iliyopita, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Riziki Abraham, alisema tangu kuanza kwa kutolewa kwa vibali vya ajira jumla ya vibali 239 vilitolewa na baadhi vimefanyiwa kazi huku vingine vipo kwenye mchakato wa kutolewa.
Alisema kwa upande wa TRA pekee walitangaza nafasi 400 ambapo jumla ya waombaji 56,815 waliwasilisha maombi.
Hata hivyo MTANZANIA ilimtafuta Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro ili kupata ufafanuzi sababu waombaji kuitwa katika awamu moja badala ya awamu tofauti ili kupunguza msongamano, lakini hakupatikana.