Na SAFINA SARWATT
- MOSHI
WAFUGAJI jamii ya Wamaasai mkoani Kilimanjaro, wameshauriwa kupunguza idadi ya mifugo waliyonayo ili kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira na migogoro ya ardhi baina yao na wakulima.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira,
wakati akizungumza na wananchi wa jamii ya Wamaasai wa Kata ya Mabogini
wilayani Moshi Vijijini, katika zoezi la kubadilishana rika kutoka
vijana kwenda uzee.
Alisema kuna haja ya jamii hiyo kuanza kufuga kisasa na kupunguza
idadi ya makundi makubwa ya mifugo ambayo yamekuwa yakiharibu mashamba ya wakulima na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.
“Kuna haja ya viongozi wa vijiji hivyo kuandaa mpango mkakati wa
kusaidia jamii hiyo ya wafugaji kuwa na shughuli mbadala za kuwaingiza kipato pamoja na idadi ndogo ya mifugo kwa kuwa ongezeko la watu limesababisha uhaba wa ardhi,” aliongeza.
kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Â Emmanuel Mzava, alisema
wameanza utaratibu wa kutenga maeneo ambayo hayajaendelezwa kwa
ajili ya malisho pamoja na kuunda kamati za kudhibiti makundi ya mifugo yanayokaa mbali na kuingizwa kwenye mashamba ya wakulima.
Baadhi ya wafugaji walieleza adha kubwa wanayoipata kipindi cha
kiangazi kuhama na makundi ya mifugo kwa ajili ya kutafuta malisho
katika mikoa jirani.